Maafisa wa serikali kuu nyanjani almaarufu National Government Administration Officers – NGAO wamehusishwa na juhudi za kuboresha viwango vya elimu nchini.
Juhudi hizo ni pamoja na mpito wa asilimia 100 wa wanafunzi kutoka kiwango kimoja cha elimu hadi kingine ambapo maafisa wa NGAO wakiwemo machifu, manaibu wao, manaibu kamishna wa kaunti, makamishna wa kaunti na hata warakibu wa maeneo huwa wanahusuika kikamilifu.
Katika kikao cha hivi maajuzi na maafisa wa NGAO, Rais Ruto aliwahimiza wapatie elimu kipaumbele katika kazi zao kwani viwango vya elimu katika maeneo yao vitatumika kutathmini utendakazi wao.
Waziri wa usalama wa taifa Kithure Kindiki naye aliangazia mchango wa maafisa hao katika sekta ya elimu akisema walitafuta wanafunzi hadi manyumbani na kuhakikisha wanakwenda shule.
Mwaka 2023, maafisa wa NGAO walifanikisha mpito wa wanafunzi wapatao milioni 1.2 hadi shule za Junior Secondary ambapo baadhi ya maafisa hao hata walizidi kiwango walichowekewa cha mpito.
Kulingana na katibu wa usalama wa taifa Raymond Omollo, maafisa wa NGAO walifanikisha mpito wa wanafunzi wapatao milioni 1.1 hadi kidato cha kwanza katika kipindi hicho hicho huku wengine elfu 15,874 kati yao wakijiunga na vyuo vya mafunzo ya kiufundi.
Ripoti ya mwaka 2022 ya benki ya dunia iliweka kiwango cha elimu kati ya watoto wa chini ya umri wa miaka15 nchini Kenya kuwa asilimia 82.88.
Maafisa wa NGAO hushirikiana pia na maafisa wa polisi kutoa ulinzi na huduma zinazohitajika wakati wa kusimamia mitihani ya kitaifa kando na kusaidia taasisi za elimu kupata vifaa vinavyohitajika.
Wasichana wanaopata mimba pia huwa wanashughulikiwa na maafisa wa serikali kuu nyanjani ambao huwa wanahakikisha kwamba baada ya kujifungua wanarejelea masomo.