Maafisa wa KRA wapata Ethanol iliyoingizwa nchini kimagendo

Marion Bosire
1 Min Read

Maafisa wa shirika la kukusanya ushuru nchini, KRA wamesema kwamba wamepata kemikali aina ya Ethanol iliyoingizwa nchini kimagendo.

Lita hizo elfu 13 za Ethanol zilipatikana ndani ya lori katika eneo la Maai Mahiu zikisafirishwa kuelekea Nairobi.

Kemikali hiyo inaaminika kuingizwa nchini kutoka nchi jirani ya Tanzania.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, KRA ilielezea kwamba mapipa 52 ya kemikali hiyo kila moja ikiwa na lita 250 yalikuwa yamefichwa kwa kutumia magunzi ya mahindi.

Dereva wa Lori hilo aliliacha na kutoroka na anasakwa na maafisa wa polisi.

Ushuru ambao ungetozwa bidhaa hiyo ambayo sasa iko mikononi mwa shirika la KRA ni takribani milioni 5.8.

Tangu mwezi Januari mwaka huu, lita 58,295 za kemikali ya Ethanol iliyoingizwa nchini kimagendo zimepatikana na washukiwa wapatao 34 kukamatwa, ulaghai ulioikosesha serikali ushuru wa hadi milioni 80.

Share This Article