Maafisa wa EACC wamkamata mshukiwa anayeuza barua bandia za kujiunga na KDF

Tom Mathinji
1 Min Read
Mshukiwa akamatwa na barua bandia za kujiunga na vikosi vya KDF.

Maafisa wa tume ya maadili na vita dhidi ya ufisadi EACC, wamemkamata mwanamume anayedaiwa kuuzia umma barua bandia za kujiunga na vikosi vya ulinzi hapa nchini KDF.

Kupitia mtandao wake wa twitter, EACC ilisema mshukiwa huyo Patrick Njue, amekuwa akiwapunja wananchi kati ya shilingi 400,000 na 500,000 ili kuwapa barua hizo bandia za kujiunga na KDF.

Njue alitiwa nguvuni mjini Sagana siku ya Alhamisi na kuhojiwa katika afisi za EACC za eneo la mlima Kenya, zilizoko mjini Nyeri.

Katika kisa kimoja, mshukiwa huyo aliitisha malipo ya shilingi 450,000 kutoka kwa mlalamishi ambaye alilipa shilingi 300,000 tarehe 11 mwezi Septemba mwaka 2023, kabla ya kukabidhiwa barua bandia ya kujiunga na vikosi vya KDF.  Alihitajika kulipa fedha zilizosalia tarehe 15 mwezi Septemba ili atie sahihi stakabadhi zilizosalia.

Walipokuwa wakimtia nguvuni, maafisa wa tume ya EACC waliwazuia watu wengine wawili ambao walikuwa wanajiandaa kulipa shilingi 500,000 kila moja, ili wapatiwe barua hizo bandia za kujiunga na KDF.

“Mtu yeyote aliye na malalamishi dhidi ya mshukiwa huyo, anahimizwa kuripoti katika afisi ya tume ya EACC iliyo karibu naye,” ilisema tume hiyo kupitia mtandao wake wa X.

Share This Article