Maafisa wa DCI wanasa mihadarati Moyale

Tom Mathinji
1 Min Read
Maafisa wa DCI wanasa mihadarati Moyale.

Maafisa wa polisi katika kaunti ndogo ya Moyale, wamenasa mihadarati iliyokuwa imefichwa katika magunia ya maharagwe,iliyokuwa ikisafirishwa katika eneo lisilojulikana.

Baada ya kupashwa habari na wananchi, maafisa wa idara ya upelelezi wa makosa ya jinai, walifika katika kituo cha mabasi ya Liban, na kupata magunia manne yaliyokuwa na maharagwe.

Walipopekua magunia hayo kwa usaidizi wa mbwa wa polisi wa kunusa, ilibainika kuwa kulikuwa na bidhaa ambazo zilitiliwa shaka.

Magunia hayo yalikuwa katika kiingilio cha kituo cha kampuni ya mabasi ya Liban, huku mmiliki wa magunia hayo akisemekana alikuwa anatafuta stakabadhi katika afisi za eneo hilo za halmashauri ya kususanyaji ushuru KRA.

Magunia hayo yalisafirishwa hadi katika afisi za maafisa wa DCI Moyale, ambako yalifunguliwa. Vifurushi 22 vya bangi vya thamani ya shilingi 435,000 vilipatikana.

Kulingana na idara ya DCI kupitia mtandao wake wa X, juhudi za kumtafuta mshukiwa aliyekuwa na magunia hayo zinaendelea.

TAGGED:
Share This Article