Maafisa 5 wa huduma za misitu watiwa nguvuni kwa madai ya mauaji

Tom Mathinji
1 Min Read

Polisi wamewatia nguvuni maafisa watano wa huduma za misitu nchini – KFS, kwa madai ya kumpiga hadi kufa mwanafunzi wa kidato cha tatu katika eneo la Maji Mazuri huko Eldama Ravine, kaunti ya Baringo.

Maafisa hao wanasemekana kumpiga hadi kufa Stephen Mwangi, mwenye umri wa miaka 19 ambaye aliingia kwenye msitu wa Narasha, kumtafuta mama yake anayedaiwa kuwekwa kizuizini na maafisa hao.

Kulingana na baba yake John Ambuka, mama huyo alikamatwa na maafisa hao akiwa kwenye harakati ya kutafuta kuni msituni humo, huku maafisa hao wakitaka kupewa hongo ya shilingi 2,000 ili kuachiliwa huru, lakini alikuwa na shilingi mia tano pekee.

Ambuka alisema ni hapo ambapo alimfahamisha mvulana huyo kuleta pesa hizo katika kituo cha Maji Mazuri ambako alikuwa akizuiliwa.

Alipowasili kwenye kituo hicho, Mwangi alimpata mama yake akidhulumiwa na makabiliano yakazuka kati yake na maafisa hao.

Maafisa hao watano wanasemekana kumshambulia Mwangi, kwa kumpiga ngumi na mateke.

Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Mogotio, Felician Nafula, alisema maafisa hao wamekamtwa huku uchunguzi ukianzishwa.

Mwangi alifariki akipokea matibabu katika hospitali ya mafunzo na rufaa ya Moi huko Eldoret kutokana na majeraha aliyopata.

Share This Article