Maadui wa Kenya wataaibika, asema Ruto

Martin Mwanje
2 Min Read

Rais William Ruto ameelezea imani kuwa mipango ya serikali yake kuibadilisha nchi hii itafaulu. 

Hili litakapotimia, Rais Ruto anasema maadui wa Kenya wataachwa wakiwa wamevaa joho la fedheha.

“Maadui wa Kenya watafedheheshwa, kwa sababu tunaenda kufaulu. Na tunaenda kuipeleka nchi hii mbele,” amesema Ruto.

“Nina imani kwamba tuna timu, watu, mpango na nia njema ya kubadilisha nchi yetu. Sina mashaka akilini mwangu, na hakuna nafasi ya kushindwa. Lazima tufaulu.”

Ruto aliyasema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini wa kandarasi za utendakazi za wizara za mwaka wa fedha 2024/2025 iliyofanyika katika Ikulu ya Nairobi leo Jumanne.

Matamshi yake yanakuja wakati ambapo viongozi wa kidini wameinyoshea serikali ya Kenya Kwanza kidole cha lawama kutokana na hulka yake ya kusema mengi bila vitendo.

Viongozi hao, wakiongoziwa na Maaskofu wa Kanisa Katoliki, wametaja mipango kama vile bima mpya ya afya ya SHIF, madeni ya iliyokuwa bima ya NHIF na mfumo mpya wa ufadhili wa vyuo vikuu kuwa ishara kuwa mambo serikalini yanakumbwa na changamoto.

Wanasema utekelezaji wa mipango hiyo umekumbwa na changamoto si haba ambazo zimetatiza Wakenya katika kupata huduma muhimu.

Aidha, viongozi wa kidini wanailaumu serikali ya Kenya Kwanza kwa kutotimiza nyingi ya ahadi zake miaka miwili baada ya kuingia madarakani.

Share This Article