Ubalozi wa China nchini Kenya uliandaa kongamano maalum Jumatatu kuadhimisha miaka 80 ya ushindi wa vita vya ukombozi wa watu wa China dhidi ya uvamizi wa Kijapani na Vita vya Ulimwengu dhidi ya Ufasisti.
Mabalozi, wawakilishi wa Wachina wanaoishi Kenya, na wasomi wa Kenya walikusanyika kuenzi historia na kusisitiza kwamba maadhimisho haya si kwa ajili ya kufufua chuki, bali ni kuhifadhi kumbukumbu, kuimarisha amani, na kuhamasisha uwajibikaji wa pamoja kwa siku zijazo.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Kaimu Balozi Zhang Zhizhong alisema ushindi wa mwaka 1945 haukuwa tu hatua muhimu kwa China, bali pia ulikuwa alama kuu katika mapambano ya dunia dhidi ya ufasisti. Alibainisha kuwa mapambano ya China yalianza mapema na kudumu kwa muda mrefu zaidi kuliko taifa lolote katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, na zaidi ya watu milioni 35 walipoteza maisha.
“Ukweli huu hauwezi kupingwa, na haustahili kusahaulika au kupotoshwa,” alisema. “Kukumbuka historia si kuendeleza chuki, bali ni kuzuia kurudiwa kwa maafa kama hayo.”
Aliongeza kuwa maonesho ya kijeshi yanayoandaliwa wakati wa kumbukumbu hilo si kwa madhumuni ya kuonyesha nguvu pekee, bali ni ishara ya dhamira ya kulinda amani.
“Njia bora ya kuwaenzi waliopoteza maisha ni kuthamini amani na kulinda mafanikio ya utaratibu wa dunia baada ya vita, ambao sasa unatishiwa na ubabe, vitisho vya upande mmoja, na kudhoofika kwa taasisi za kimataifa,” alionya.
Kwa upande wake, Bw. Gao Wei, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wachina wanaoishi Kenya, alitoa heshima ya kihisia kwa walioteseka wakati wa vita.
“Taifa linalosahau historia yake hupoteza mwelekeo,” alisema, akisisitiza kuwa kusudi la kukumbuka si kuendeleza chuki, bali ni kupata nguvu ya kusonga mbele.
Aliongeza kuwa historia hiyo ya majonzi ni ukumbusho kwamba uvamizi huzaa maafa, na amani haipaswi kuchukuliwa kwa mzaha.
“Kutokana na historia hiyo ya kusikitisha, tulijifunza masomo matatu ya kudumu: mshikamano ni nguvu, ujasiri huleta heshima, na nguvu huhakikisha amani,” alisema.
Akisimulia mawazo yake katika gwaride la kijeshi lilifanyika Beijing, Gao alieleza kuwa nidhamu ya wanajeshi na teknolojia ya kisasa ni ushahidi wa uimara wa China. Hata hivyo, alisisitiza kuwa maana ya kweli ipo katika kujitolea muhanga kwa waliopoteza maisha.
“Bendera ikipanda na wimbo wa taifa ukipigwa, nilikumbushwa kuwa historia haipaswi kusahaulika, na amani lazima ilindwe,” aliongeza.
Profesa Peter Kagwanja, rais wa taasisi ya sera za Afrika – Africa Policy Institute, alihusisha mchango wa China katika vita hivyo na historia ya dunia, akisema kuwa katika miongo minane iliyopita, binadamu wameushinda ufasisti, ukoloni, na ubaguzi wa rangi, lakini changamoto mpya kama ubinafsi wa kitaifa, ulinzi wa masoko, na mabadiliko ya tabianchi zinatishia mshikamano wa kimataifa.
Alifananisha China na “jitu lenye upole” lililoinuka kwa amani na kufanikiwa kiuchumi duniani, pia likiwa na jeshi kubwa.
“Maendeleo ya amani yameibadilisha China kuwa uchumi wa pili kwa ukubwa duniani, ikiwa na bajeti ya ulinzi ya dola bilioni 314 mwaka 2024 – ya pili duniani na inayochukua asilimia 12 ya matumizi ya ulinzi duniani,” alisema.
Akinukuu maneno ya Rais Xi Jinping kwamba “China haizuiliki” na “haiwezi kutishwa na mababe,” alisisitiza kuwa nguvu za China ni dhamana ya amani, si za uchokozi.
Dkt. Hassan Khannenje, mkurugenzi wa taasisi ya kimataifa ya masuala ya kistratejia ya pembe ya Afrika – Horn Institute, alionya dhidi ya juhudi za kupuuza mchango wa China katika ushindi wa Muungano dhidi ya ufasisti. Alikosoa wale wanaopuuza historia hii kama “vita vya simulizi” huku wakibeza ukweli na gharama ya kibinadamu iliyolipwa.
“Leo, tupo katika njia panda ya kihistoria, ambapo kuna mapambano kati ya wanaotaka kudumisha mfumo wa mabavu, ubabe wa kifedha, na upotoshaji wa historia kwa upande mmoja, na wale wanaotafuta dunia yenye usawa na ustawi wa pamoja kwa upande mwingine,” alisema.
Alihimiza China na mataifa ya Kusini – Global South, kuongoza katika juhudi za kujenga dunia ya ushirikiano wenye haki, ikilinda utaratibu wa baada ya vita.
Profesa Thomas Namwamba wa Chuo Kikuu cha Kenyatta aliongeza kuwa nafasi ya China kama mshirika wa maendeleo barani Afrika ni ushahidi kwamba taifa hili limejitolea kwa ustawi wa binadamu na utulivu wa dunia.
“China inaendelea kupanua nafasi yake ya kimaadili kusisitiza ukweli wa kihistoria na kutetea haki za kimataifa.” alisema
Kwa upande wake, Profesa Patrick Maluki wa Chuo Kikuu cha Nairobi alisisitiza kuwa ushindi dhidi ya ufasisti ni funzo muhimu linalotoa fundisho kuwa utawala wa dunia lazima ujengwe juu ya usawa, ushirikiano, na heshima ya pande zote.
“Kulitambua hili si suala la uhalisia wa kihistoria pekee, bali pia ni wajibu wa kimaadili. Ili kuheshimu historia kwa ukamilifu, lazima tusikilize sauti zote na kukumbuka kafara zote,” alisema.
Katika hotuba zote, ujumbe wa pamoja ulisikika wazi: Maadhimisho ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia si kwa ajili ya kufufua uhasama wa zamani, bali ni kuenzi mashujaa, kulinda ukweli wa kihistoria, na kupata nguvu ya kukabiliana na changamoto za leo.
“Historia ni mwalimu bora zaidi,” alisema Gao Wei.