Maadhimisho ya Siku ya Redio Ulimwenguni

Februari 13 ilichaguliwa kuwa siku ya redio ulimwenguni kwani ndiyo siku kituo cha redio cha Umoja wa Mataifa kiliasisiwa mwaka 1946.

Marion Bosire
2 Min Read

Leo Februari 13, 2025 ni Siku ya Redio Ulimwenguni, siku ambayo huadhimishwa kila mwaka kama njia ya kutambua uwezo mkubwa wa redio kama chombo cha mawasiliano.

Siku hii ilitengwa pia kwa ajili ya kukuza uhuru wa kujieleza, upatikanaji wa habari na kukuza maelewano kati ya jamii tofauti.

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilitenga rasmi siku hii ya redio mwaka 2011 na maadhimisho ya kwanza yakafanyika mwaka uliofuata wa 2012.

Maadhimisho haya hutoa fursa ya utathmini wa jukumu muhimu la redio katika mawasiliano ulimwenguni, elimu na maendeleo ya jamii.

Shirika la utangazaji nchini KBC limekuwa likiandaa hafla za kuadhimisha siku hii muhimu kuanzia Jumatatu Februari 10, 2025 ambapo watangazaji wa redio wa vituo mbali mbali wamekuwa wakikata keki na kufurahikia wiki hii.

Na leo siku ambayo inatizamiwa kuwa kilele cha sherehe hizo, watangazaji hao walivaa shati tao za rangi ya kijani ili kuwiana na kauli mbiu ya mwaka huu ambayo ni “Redio na mabadiliko ya tabianchi”.

Akihutubia wafanyakazi wa shirika la KBC jana, Mkurugenzi Mkuu Agnes Kalekye alisimulia jinsi upeperushaji wa habari kuhusu mafuriko ya Tana River uliwezesha kuhamishwa kwa watu waliokuwa wakiishi katika maeneo hatari.

Asili ya redio inahusishwa na mvumbuzi wa Kiitaliano Guglielmo Marconi wa karne ya 19, ambaye alifanikiwa kutumia mawimbi ya redio juu ya Bahari ya Atlantiki mwaka 1901.

Kazi ya Marconi ilibadilisha mawasiliano kwa kuweka misingi ya utangazaji wa redio ambao uliimarika hata zaidi katika karne ya 20.

Februari 13 ilichaguliwa kuwa siku ya redio ulimwenguni kwani siku hiyo mwaka 1946 ndiyo kituo cha redio cha Umoja wa Mataifa kiliasisiwa.

Mwaka huu, watangazaji wa redio wanahimizwa kutumia majukwaa yao ya kikazi kuhamasisha umma kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, athari zake na namna ya kukabiliana nazo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *