Redio ni chombo muhimu kinachofahamika cha mawasiliano ambacho kimekuwepo kwa zaidi ya Karne moja.
Maadhimisho ya siku ya redio ulimwenguni yakitarajiwa kuandaliwa Februari 13, 2025, maudhui yakiwa “Redio na mabadiliko ya tabianchi” wanahabari wanahimizwa kuangazia maswala ya mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza katika afisi yake mjini Meru, Mratibu wa Baraza la vyombo vya habari nchini MCK wa eneo la kati na mashariki mwa nchi Jackson Karanja, alisema vyombo vya habari ni muhimu.
Tunapoadhimisha siku ya redio ulimwenguni, Karanja anahimizawanahabari kuangazia kile ambacho redio inafanya, inachostahili kufanya na kile ambacho ni lazima ifanye ili kushughulikia mabadiliko ya tabianchi.
Karanja alisema redio ambayo ndiyo chombo cha mawasiliano kinachotumiwa na wengi, na sasa kuna vituo zaidi ya 300 vilivyosajiliwa vya redio nchini vikiwemo vya lugha asilia, inafaa kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mratibu huyo alisema watu wanapozungumzia hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, wengi huwazia upanzi wa miti lakini hiyo ni njia moja tu.
Aliwataka watangazaji wa redio kuwazia kuandaa simulizi za kina kuhusu njia nyingine za kutunza mazingira kama vile usimamizi bora wa taka na kutumia tena taka za plastiki.
Ushauri wake kwa watangazaji hao ni kutoangazia tu kuripoti kuhusu majanga ya kimazingira yanapotokea kama vile mafuriko na njaa na badala yake watoe suluhu za kuzuia majanga hayo.