Maaafisa wa afya wanagenzi wapigwa kumbo na mahakama

Martin Mwanje
1 Min Read

Ni pigo kwa maafisa wa afya wanagenzi ambao wamekuwa wakipigania malipo bora nchini. 

Hii ni baada ya Mahakama ya Wafanyakazi huko Uasin Gishu kudumisha viwango vya malipo ya maafisa hao vilivyowekwa na Tume ya Mishahara na Marupurupu, SRC mapema mwaka huu.

Maafisa hao kupitia kwa Chama cha Madaktrari cha KMPDU na taasisi zingine za kitaaluma waliwasilisha kesi mahakamani Machi 13, 2024 wakipinga vikali viwango hivyo kwa misingi kwamba SRC haikutafuta ushauri wao wala haina mamlaka ya kuweka viwango hivyo.

Kwenye kesi vilivyowasilisha mahakamani, vyama hivyo vilitaka viwango hivyo vibatilishwe.

Hata hivyo katika uamuzi wake, Mahakama ya Wafanyakazi imebaini kuwa SRC ilitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa katiba kwa kuzingatia uhalisia wa bajeti ya nchi na hali ya kipekee ya mafunzo ya programu za uanagenzi.

Kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa na SRC, maafisa wanagenzi wa tiba, wanafamasia na maafisa wanagenzi wa meno watakuwa wakilipwa kati ya shilingi 50,000-70,000 huku maafisa wanagenzi wa uguzi walio na shahada wakilipwa kati ya shilingi 35,000- 50,000 sawia na wenzao wa kliniki walio na shahada.

Maafisa wa kliniki walio na stashahada watakuwa wakilipwa kati ya shilingi 25,000-35,000.

 

Share This Article