Mwigizaji wa hapa nchini Lupita Nyong’o, amezindua kampeni ya kutafuta fedha kufadhili utafiti wa ugonjwa wa fibroids ambao husababisha uvimbe kwenye nyumba ya uzazi kwa wanawake.
Licha ya kuwa Nyong’o aliugua ugonjwa huo mwaka 2014, alitangaza hali yake mara ya kwanza hadharani mwaka 2025, mwaka ambao alipokea tuzo la Oscar kutokana na jukumu lake kwenye filamu ya ‘12 Years a Slave’.
Akizungumza kwenye mahojiano ya awali, Lupita alisema alijihisi kupata aibu kutokana na hali hiyo, huku akiwa na wasiwasi kuhusu afya yake ya uzazi.
Tangu wakati huo, Lupita mwenye umri wa miaka 42 amekuwa balozi wa afya, huku akitoa hamasisho kuhusu afya ya wanawake.
Mwigizaji huyo alikiri kutamaushwa kwamba madaktari hawakuelezea chanzo halisi cha ugonjwa wa fibroids, wakimweleza alipaswa kufanyiwa upasuaji au aendelee kuishi kwa maumivu. Aidha walimweleza kuwa hata kama atafanyiwa upasuaji, huenda akaugua ugonjwa huo siku za usoni.
“Sasa miaka 12 baadaye nimeugua fibroids tena….nimeongeza maradufu kiwango cha fibroids na nimefahamishwa chaguo ni mbili tu, kufanyiwa upasuaji au kuishi kwa maumivu,” alisema Lupita.
Aidha, alisema alivunjwa moyo baada ya kugundua kuwa wanawake wengi hutolewa kabisa nyumba ya uzazi, huku akiwahimiza wanawake kutafuta ushauri wa pili kabla ya kuchukua uamuzi huo.
“Kuna nguvu nyingi katika kuzungumza…nilizungumza kuhusu hali yangu na baada ya kufahamu wanawake kadhaa wanaugua fibroids, niliona siko peke yangu,” aliongeza mwigizaji huyo