LSK: Uteuzi wa jopokazi la kuchunguza deni la taifa ni ukiukaji sheria

Tom Mathinji
2 Min Read

Chama cha wanasheria hapa nchini LSK, kimepinga hatua ya Rais William Ruto ya kubuni jopokazi la kufanya ukaguzi wa deni la taifa hili, kikitaja hatua hiyo ukiukaji wa sheria.

Hayo yanajiri siku moja tu baada ya Rais Ruto kuwateua wanachama wa jopokazi hilo, akiwemo Rais wa chama cha LSK Faith Odhiambo.

Afisa mkuu mtendaji wa LSK Florence Muturi, alisema afisi ya Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali ndiyo iliyo na mamkala ya kukagua deni la taifa.

“Kwa kuzingatia sehemu ya 229 ya katiba ya Kenya, maoni yetu ni kwamba hatua ya kubuni jopokazi hilo ni kinyume na katiba. Jukumu la ukaguzi wa deni la taifa ni la Mkaguzi mkuu wa hesabu za umma,” alisema afisa mkuu mtendaji wa LSK Florence Muturi.

Ni kutokana na msingi huo ndiposa chama hicho  kimemtaka Rais wake Faith Odhiambo kukataa uteuzi wa Rais William Ruto katika jopo hilo.

Muturi alisema chama hicho kimeazimia kuwa hakuna mwanachama wake atakubali uteuzi katika jopo hilo.

Rais William Ruto siku ya Ijumaa aliwateua wanachama wa Jopokazi hilo, ambalo mwenyekiti wake ni Nancy onyango.

Wanachama wengine walioteuliwa ni pamoja na Prof. Luis G. Franceschi ambaye atakuwa mwenyekiti wa jopokazi hilo, Rais wa chama cha mawakili nchini (LSK) Faith Odhiambo, mwenyekiti wa ICPAK Phillip Kaikai, Rais wa chama cha wahandisi nchini Shammah Kiteme, na mtaalam wa sera na uongozi Vincent Kimosop.

Jopokazi hilo linatarajiwa kuchunguza deni la taifa na kutoa ripoti yake baada ya miezi mitatu.

Akiteua jopokazi hilo, Rais William Ruto, alisema deni la taifa linazidi kuibua wasiwasi hapa nchini, na hivyo ipo haja kwa wananchi kufahamishwa kuhusu deni hilo na jinsi rasilimali za umma zilivyotumiwa.

Hatua hiyo ya Rais ilijiri baada ya wakenya kupinga Mswada wa Fedha 2024, ambao alikataa kuutia saini na badala yake kuurejesha bungeni kwa mwongozo zaidi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *