Louis van Schoor anayedaiwa kuwaua watu wasiopungua 39 Afrika Kusini wakati wa enzi za ubaguzi wa rangi, ameaga dunia.
Mzee huyo wa miaka 72 almaarufu “Apartheid Killer”, alikuwa akipokea matibabu ya mguu hospitalini.
Kulingana na familia yake, Schoor alifariki Alhamisi mchana baada ya kuambukizwa bakteria.
Kifo hicho cha Schoor, kimejiri wiki moja tu baada ya shirika la utangazaji la BBC kuanzisha uchunguzi kuhusu maisha yake ya awali uliofichua maelezo mapya ya mauaji aliyotekeleza katika miaka ya 80.
Dada ya mmoja wa waathiriwa wake aliambia shirika la BBC kuwa anatumai polisi watafungua upya kesi hizo kwa uchunguzi licha ya kifo chake.
Wakati ambapo mfumo wa kibaguzi uliweka uongozi mkali uliowapa upendeleo Waafrika Kusini weupe, Van Schoor alikuwa akifanya kazi kama mlinzi wa kibinafsi katika jiji la pwani la London Mashariki.
Kati ya 1986 na 1989, alipiga risasi na kuwaua watu wasiopungua 39. Waathiriwa wake wote walikuwa weusi na mwenye umri wa chini zaidi alikuwa na miaka 12.