Lizzo kushtaki waliokuwa wacheza densi wake

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Marekani Lizzo anapanga kuwashtaki waliokuwa wacheza densi wake baada yao kumshtaki.

Crystal Williams, Arianna Davis na Noelle Rodriguez, walimshtaki Lizzo, kampuni yake iitwayo  Big Grrrl Big Touring, Inc na msimamizi wake wa densi Shirlene Quigley, mwanzo wa mwezi huu kwa kile walichokitaja kuwa dhuluma za kingono, mazingira mabaya kikazi na kuwaaibisha kutokana na maumbile yao.

Watatu hao wanadai kwamba Lizzo aliwalazimisha kugusa watu ambao walikuwa wakicheza densi uchi kwenye eneo moja la burudani huko Amsterdam mwezi Februari. Wanasema pia kwamba walihudhuria tamasha nyingine huko Paris mwezi Machi ambayo hawakujua ilihusisha kucheza densi uchi.

Wakili wa Lizzo aitwaye Marty Singer, hata hivyo anapinga dai hilo akisema ana ushahidi wa picha na video kutoka kwa tamasha hiyo ya Machi 5 jijini Paris ufaransa ambazo zinaonyesha kinyume kabisa cha dai lao.

Singer anasema kesi dhidi ya mteja wake haina msingi wowote na wanapanga kushtaki walalamishi punde baada ya kesi yao kukamilika na Lizzo kuondolewa makosa.

Awali Lizzo kupitia Instagram alijitetea kuhusu kushtakiwa na wacheza densi hao watatu akisema maadili yake ya kikazi na heshima vimetiliwa shaka na kwa kawaida yeye huwa hajibu madai ya uongo lakini madai hayo ni ya kushangaza sana na hayawezi kunyamaziwa.

Wakili wa Crystal, Arianna na Noelle kwa jina Ron Zambrano anadai kwamba kufikia sasa, walalamishi wengine sita wamejitokeza wakitaka kujumuishwa kwenye kesi hiyo dhidi ya Lizzo.

Kikao cha kesi hiyo kimepangiwa kuandaliwa Januari 26, 2024.

Kesi hiyo imeathiri Lizzo kikazi ambapo tamasha ya “Made In America” ambayo angekuwa mtumbuizaji mkuu pamoja na SZA imetupiliwa mbali.

Share This Article