Lita 750 za Ethanol zanaswa Kiambu

Marion Bosire
2 Min Read

Shirika la kupambana na matumizi ya pombe na mihadarati nchini, NACADA limenasa lita 750 za kemikali aina ya Ethanol katika nyumba moja huko Ruaka, kaunti ya Kiambu.

Shughuli hiyo ilifanikishwa kufuatia operesheni iliyotekelezwa jana Jumatano usiku na kundi la maafisa wa taasisi mbalimbali wakiwemo maafisa wa NACADA, polisi na maafisa wa shirika la kukusanya ushuru nchini, KRA.

Kundi hilo lilikuwa limepokea habari kuhusu kuwepo kwa kemikali hiyo mahali hapo ambapo pia walipata mitungi 40 ya lita 250 kila mmoja iliyokuwa tupu na inaaminika ilikuwa na kemikali ya Ethanol.

Inaaminika kwamba kemikali iliyokuwa kwenye mitungi hiyo ilipakiwa upya na kusafirishwa kwa ajili ya matumizi kinyume cha sheria.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya tukio la kaunti ya Kirinyaga ambapo wanywaji pombe walifariki na wengine wanapokea matibabu baada ya kubugia pombe ghushi.

Mkurugenzi Mkuu wa NACADA Dkt. Anthony Omerikwa alionya kupitia taarifa kwamba unywaji wa pombe haramu ambayo haijaidhinishwa ni hatari kwa afya na huenda ukasababisha madhara kama kupofuka na hata kifo.

Kulingana na Omerikwa, shirika la NACADA linaendelea kushirikiana na maafisa mbalimbali wa serikali kuu na wa usalama kutekeleza operesheni za kukabiliana na pombe ghushi na haramu.

Operesheni hizo alisema zitaendelea kote nchini na yeyote atakatepatikana na hatia atachukuliwa hatua za kisheria.

Wananchi wanaombwa kujuza maafisa husika kuhusu utengenezaji, usambazaji na uuzaji wa pombe inayoshukiwa au dawa nyingine za kulevya.

Share This Article