Lebanon yataka Israel iondoke kwenye himaya yake

Rais wa Lebanon, Joseph Aoun alisema nchi yake inakabiliwa na changamoto za Israel kukalia ardhi yake na kuingiliwa na mataifa ya kigeni.

Marion Bosire
2 Min Read

Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, ameitaka Israel kuondoa vikosi vyake kusini mwa Lebanon.

Kiongozi huyo pia ameishutumu Iran kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo kupitia makundi yenye silaha yanayofanya kazi nje ya mamlaka ya serikali.

Akizungumza Jumamosi, Novemba 21, Aoun alisema nchi hiyo inakabiliwa na changamoto mbili kuu.

Moja ni Israel kukalia sehemu ya ardhi yake na ya pili ni kuingiliwa na mataifa ya kigeni kupitia viongozi wenye ushawishi ndani ya utawala wa Iran.

Alisema changamoto hizo zinadhoofisha mamlaka na uhuru wa Lebanon, hivyo kuizuia sherehe kamili ya uhuru wake.

Akiielekeza ujumbe wake kwa Israel, Aoun alitaka vikosi vyake kuondoka katika kila sehemu ya ardhi ya Lebanon, kusitisha mashambulizi na kuwaachilia huru raia wa Lebanon wanaoshikiliwa katika vituo vya mahabusu vya Israel.

Pia alisisitiza dhamira ya serikali yake ya kuhakikisha silaha zote zinawekwa chini ya udhibiti wa serikali, akisema hakuna kundi lenye silaha linalopaswa kufanya kazi nje ya mamlaka ya taifa au kutumikia maslahi ya mataifa ya kigeni.

Matamshi hayo yanajiri wakati juhudi za kupokonya kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran silaha, zikiwa zimekwama.

Makubaliano yaliyofikiwa Juni kupitia upatanishi wa Marekani yalilenga kupokonya Hezbollah silaha, kuondoa vikosi vya Israel kusini mwa Lebanon na kupeleka wanajeshi wa Lebanon katika eneo hilo.

Hata hivyo, utekelezaji umekwama kutokana na Hezbollah kukataa kusalimisha silaha zake, huku Israel ikiendelea kufanya mashambulizi ya kijeshi nchini Lebanon.

Share This Article