Mwanamuziki wa Marekani Lauryn Hill amejiondolea lawama kuhusu makosa yaliyofanyika katika tamasha la Essence la mwaka huu.
Msanii huyo alichelewa kuingia jukwaani kwa muda wa masaa mawili na alipoingia, akadumu muda wa saa moja pekee. Waandalizi wa Essence Festival hata hivyo waliomba msamaha kuhusu tukio hilo.
Baadaye Lauryn aliyumia akaunti yake ya Instagram kuelezea kwamba makosa hayakuwa yake na hajayumbishwa kwa vyovyote vile na tukio hilo.
Alianza kwa kushukuru Essence kwa kuomba msamaha akisema kwamba maisha yake yanaendelea kama kawaida, anahudhuria matamasha kila anapohitajika na hajali kuhusu lolote kwani yeye ni wa muhimu.
“Wanafamilia naomba nizungumzie masuala kadhaa, ninahusika katika kila hatua ya maandalizi ya matamasha yangu kwa sababu inahitajika hivyo ili kulinda uadilifu wa ujumbe wangu na ubora wa kazi yangu,” aliandika Hill.
Kulingana naye, yeye hujitolea kuhusika katika hatua zote husika huku akiendelea na maisha yake mengine kama mzazi, mtu aliye na wajukuu na mtunzi wa familia yake.
“Ninafanya haya yote bila kulalamika kwa sababu ya upendo na ili niweze kutumbuiza kwa muziki faafu kwa wanaonisikiliza” aliendelea kuelezea.
Msanii huyo anafahamika kwa kuchelewa kila mara kufika jukwaani kwa matamasha kadhaa lakini anasema sio kweli na kwamba ni dhana tu watu wako nayo kumhusu akiitaja kuwa potovu.
“Jiulize ni vipi na ni kwa nini nimeweza kuendeleza kazi yangu kwa miaka mingi huku kukiwa na juhudi za kuniharibia sifa,” alijitetea Hill.
 
					 
				 
			
 
                                
                              
		 
		 
		 
		