Kaunti ya Kwale ambako sherehe za mwaka huu za Mashujaa zinaandaliwa ina idadi ya watu 886,820. Hii ni kulingana na zoezi la kuhesabu watu lililotekelezwa mwaka 2019.
Eneo hilo la Pwani ya Kenya linapakana na Bahari Hindi upande wa Mashariki, kaunti ya Taita Taveta upande wa Magharibi na Tanzania upande wa Kusini.
Shughuli za kiuchumi za wakazi wa kaunti hii zinajumuisha kilimo, uvuvi, uchimbaji madini na utalii.
Miji inayopatikana kaunti ya Kwale ni Kwale mjini, Diani, Ukunda na Msambweni.
Kaunti ya Kwale ina maeneo bunge manne; Matuga, Kinango, Lunga Lunga na Msambweni.
Jamii kubwa za kaunti hii ni Digo na Duruma ambazo ni sehemu ya Mijikenda. Jamii hizi zimedumisha utamaduni wao unaojumuisha uzungumzaji wa lugha za Kiswahili na Kidigo.
Vile vile, kaunti ya Kwale ina rasilimali muhimu ambazo hupiga jeki maisha ya wakazi kiuchumi na pia kijamii.
Rasilimali hizo ni madini aina ya Titanium, msitu wa Shimba Hills na uvuvi katika Bahari Hindi.
Utalii pia haujaachwa nyuma katika kaunti ya Kwale. Kwa muda mrefu, vivutio vya utalii vya kaunti hiyo vimepata sifa sufufu na kuwakaribisha wageni kutoka pembe zote za nchi, Afrika na ulimwengu kwa jumla.
Vivutio hivyo ni pamoja na ufuo wa Diani, mbuga ya Shimba Hills, mbuga ya Kisite-Mpunguti na Majimoto Springs.
Sherehe za kitamaduni katika kaunti ya Kwale huongozwa na wazee wa Kaya.