Kundi la wanawake la Paran lililo na makao yake makuu katika eneo la Ololunga Kaunti ya Narok, limesimama kama taa ya matumaini katika utunzaji wa mazingira na uwezeshaji wa wanawake.
Tangu kuasisiwa kwake mwaka 2005, kikundi hiki ambacho kimeundwa na vikundi 64 za wanawake kutoka jamii asili za Maasai na Ogiek kimeibuka kuwa mfano bora wa jinsi jamii za mashambani hasa wanawake wa jamii za asili walivyogeuza changamoto kuwa fursa, na mazingira kuwa msingi wa matumaini mapya. Hii ndiyo simulizi ya Paran Women Group, kikundi cha wanawake waliokataa kukaa kimya huku mazingira yao yakiharibika, na badala yake wakasimama kuwa walinzi wa ardhi yao na sauti ya mabadiliko.
Kwa msukumo wa kutaka kusimulia juhudi za kijasiri za kuhifadhi mazingira zinazoongozwa na jamii mashinani, nilifunga safari kutoka jiji la Nairobi hadi Ololunga, eneo bunge la Narok Kusini, Kaunti ya Narok, nikitaka kujionea kwa macho kazi inayofanywa na kundi hili la kina mama la Paran.
Safari yenyewe ilikuwa ya kuvutia, nilifurahia kuona mila na mitindo ya kipekee ya maisha ya jamii ya Maasai, ikiambatana na mandhari ya nyanda za savana, vilima vilivyopinda kwa upole na upepo wa matumaini ukinong’ona kwenye majani, taswira kamili ya safari ya wanawake wengi wa vijijini kuelekea uimara na uongozi wa kimazingira.
Nilipowasili kwenye makao makuu ya Paran Women Group Resource Centre Ololunga, nilikumbana na mazingira ya ufanisi na mshikamano. Wasichana wachanga walifanya kazi kwa mikono yao kwa bidii na tabasamu usoni, wakichochewa na matumaini ya kubadilisha maisha yao na ya vizazi vijavyo. Walionekana wakihudumia miche kwenye moja ya vitalu vya miti vya kikundi, kwa uangalifu na ari ya hali ya juu.

Hili lilikuwa onyesho dhahiri la uelewa wao kuhusu nafasi ya miti katika kuhifadhi mazingira yao. Hii ilikuwa njia rahisi lakini yenye maana kubwa ya kuelewa kazi ya kikundi hiki, shughuli ya moja kwa moja, inayohusisha vijana, na yenye malengo ya kudumu.
Tulilakiwa kwa ukarimu na Bi. Naiyan Kiplagat, Mkurugenzi wa kikundi na mmoja wa viongozi mashuhuri wa uhifadhi unaoongozwa na jamii. Kwa sauti ya utulivu lakini thabiti, alianza kusimulia safari ya Paran. Tangu alipoanza kusimulia historia ya kikundi na mafanikio waliyoyapata, ilikuwa wazi kuwa ana ari isiyo na kifani.
“Tulipoanza 2005, mazingira yetu Narok yalikuwa yameharibika sana, kwasababu wildfires ambayo haungejua inatoka wapi ilikuwa inaingia msituni na kwa mashamba ya watu na kufyeka na kuchoma kila kitu na ile miti ya zamani ya madawa na kila kitu ilifagia kabisa. Tukianza hakukuwa na miti eneo hili” Alisema Naiyan Kiplagat.
“Mwaka wa 2005 tuliathirika sana na mambo ya climate change, huku miti ilikuwa imekatwa yote na visiki ndo zilikuwa zimebaki’ tulipokuja pamoja tukasema kila mama aanze kupanda miti kwake, na tulikuwa na merry go rounds ya kupanda miti”
“Kwasasa hata ukisimama, huwezi ona boma ya mtu imefunikwa na miti na tumeweza kufanya kazi kwelikweli kuhakikisha kila boma imefunikwa na miti na kila boma inapanda miti kwake’ aliongeza, Jambo ambalo binafsi kama mwanahabari nilithilibitisha.
Chini ya uongozi wake, kikundi hiki cha Paran Women Group kimekuwa sauti muhimu katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuinua nafasi ya wanawake, si tu katika Kaunti ya Narok bali pia katika maeneo mengine.
“Kitu ambacho kinatupeleka mbele kama Paran Women Group ni umoja na kufanya kazi kwa pamoja, anasema Naiyan Kiplagat “ikiwa ni maji na mambo ya tree nursery tunafanya pamoja na ndio maana unaona imefaulu hivi”
“Kuna zile events za Kalenda kama World Environmental Day, World tree planting day , tumefanya watu waelewe kwamba hizi ni siku muhimu ambayo inatakikana tufanye restoration ya miti, sisi kama Paran Group, tunafuatilia hizo siku za calender sana kutoa hamasa” alisema.
Lengo kuu la kikundi hiki ni uhifadhi wa mazingira. Wamekuwa mstari wa mbele katika upandaji miti ndani na karibu na msitu wa Mau, mojawapo ya vyanzo vikuu vya maji nchini Kenya. Kufikia sasa, kimepanda zaidi ya miche 100,000 ya miti asilia Kupitia kampeni shirikishi za jamii.
“Tuna vituo vingine 21 vya kuhifadhi miche za kina mama katika vituo vyetu 7 vingine kando na hiki’ kama msitu wa MAU ambao tunaendelea kuupanda miti , kati ya ekari 200 tumemaliza ekari 100 kwa kupanda miti 100, 000 ya miti asilia , na kutoka mwaka wa 2005 kufikia sasa kwasababu tumepanda miti majumbani, mashuleni, na huko MAU pia tumepanda zaidi ya miti milioni 3 kila mahali (kwa jumla)” alisema Naiyan Kiplagat.
Juhudi hizi si tu zinarejesha uoto wa asili, bali pia zinahakikisha upatikanaji wa maji kwa jamii zinazotegemea misitu hiyo na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kurejesha maeneo yaliyoharibiwa, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa jamii na mifumo ya ikolojia.

Hata hivyo, mafanikio haya hayajapatikana bila changamoto. Wanakikundi hukumbana na uhaba mkubwa wa maji, hali inayowalazimu wanawake kutembea mwendo mrefu hadi mto Ewaso Nyiro kubeba maji kwa ajili ya kunywesha miche. Kila tone la maji linabebwa kwa bidii na matumaini, likiwakilisha si tu juhudi za kuhifadhi mazingira, bali pia ushuhuda wa uvumilivu wa wanawake hawa jasiri.
“Shida tuliyonayo kubwa ni maji kama kina mama, tuna matangi mawili ya lita 10000, lakini hazitoshi, kutokana na activities nyingi tulizonazo hapa’ mto ambao uko karibu ni Ewaso Nyiro lakini bado ni mbali ni kati ya mita 500 hadi 1000 (kutoka hapa makao makuu ya Paran) na inakuwa ngumu kwasababu wakiendea maji asubuhi wanarudi jioni na wakati mwingine wakienda jioni wanarudi saa sita usiku.” Bi, Naiyan alinieleza. Kwahivyo hii imekuwa changamoto kubwa na hiyo maji bado haiwezi ikatosha.
Athari za kazi ya kikundi hiki zimeenea katika maeneo mengine. Kando na kituo cha Ololunga, kikundi hiki kina vituo vingine saba vya rasilimali katika maeneo mbalimbali, ambavyo vimewezesha huduma zao za uhifadhi na uwezeshaji ili kufikia jamii nyingi zaidi zilizo karibu na maeneo ya misitu. Kabla ya kuanzisha kituo chochote, kikundi huandaa vikao vya majadiliano na jamii, ambapo kinawaelimisha kuhusu umuhimu wa kuhifadhi misitu, hatari za mabadiliko ya tabianchi, na mbinu shirikishi za kushughulikia changamoto hizi. Njia hii jumuishi imesaidia kuimarisha ushirikiano na kumiliki mchakato wa uhifadhi na maendeleo.
“Kwanza kabla ya kufanya restoration huwa tunaandaa vikao na jamii na kuwaeleza kuhusu Mabadiliko ya tabianchi na nini ambacho tunaweza kufanya kujikinga na madhara haya” katika sehemu zilizo karibu na msitu tulianzisha activities nyingi na ambazo ni rafiki kwa mazingira na ni vitu ambazo zitawapatia Pesa na kuwa na chakula cha kutosha kwa boma zao” na hata sahi wanaendelea na shughuli hizo na wameelewa kuendelea kukata miti watakuwa na madhara mabaya na wanaendelea kuelimisha wengine kuwa kukata miti ni vibaya” akasema Naiyan Kiplagat.
Mbali na upandaji miti, kikundi hiki kinahamasisha matumizi ya nishati mbadala kama jiko za kupunguza matumizi ya kuni, hatua inayosaidia kuhifadhi misitu na kuboresha afya za familia. Pia wanahamasisha kilimo rafiki kwa mazingira, ambacho huwasaidia wakulima hasa wanawake kuboresha afya ya udongo na kupata chakula cha kutosha.
“Tunawasaidia wamama na kuwafundisha kuiga mbinu mpya za zitakazowasaidia kuongeza mazao katika mashamba yao” Bernard Makinia alinieleza katika mahojiano yetu huku akisisitiza umuhimu wa wanaume katika mradi kama huu.
Lakini zaidi ya yote, Paran wanathamini na kutumia maarifa ya jadi kama vile kutabiri hali ya hewa kupitia mawingu na upepo.
“Tunatambua dalili za mvua kwa kuangalia kama kuna mawingu kwa macho au mvua itaanguka hiyo ndio tunatumia,” anasema Bi. Naiyan. “bado hatujashirikiana sana na idara ya utabiri wa hali ya hewa” . Lakini tukishirikiana na wataalamu wa hali ya hewa, tunaweza kuoanisha maarifa ya jadi na kisayansi na kuwa na maandalizi bora zaidi.”
Mchanganyiko huu wa hekima ya kiasili na sayansi ya kisasa ni moja ya mifano ya namna ambavyo suluhisho la kimazingira linaweza kuwa la ndani, bunifu, na endelevu.
Jitihada za kikundi pia zimeunganishwa na uwezeshaji wa wanawake na vijana. Miradi yao ya kijamii na kiuchumi inajumuisha ufugaji wa nyuki, utengenezaji wa mkaa mbadala, na ususi wa shanga, ambayo hutoa chanzo cha mapato huku ikihimiza uwajibikaji kwa mazingira. Aidha, kikundi kinasaidia uanzishaji wa bustani za nyumbani/jikoni, zinazosaidia familia kupata lishe bora na kipato cha ziada.
“Tulipoketi mwaka 2005 tulisema ni vizuri kuwa na shughuli za kina mama waweze kupata kitu kidogo na kupata chakula, na tukawa na maono tofauti tofauti kulingana na mahali wamama wanakotoka, kina mama wanaoishi ndani sana walisema wanaweza kufanya kazi ya ufugaji wa nyuki na kutengeneza shanga, wengine wakasema wanaweza kupanda chakula kupitia bustani za nyumbani” hizi kazi ambazo tulianza huo mwaka zimewasaidia sana na tumeona visa vya mimba ya mapema vimepungua” anasema Naiyan
Mbali na kuwezesha kiuchumi, Paran pia kimeanzisha kituo salama kwa wanawake, ambacho huwasaidia wanawake waliokumbwa na ukatili wa kijinsia, ndoa za mapema, na changamoto nyingine za kijamii.
Kituo hiki hutoa makazi ya muda, ushauri wa kisaikolojia, msaada wa kisheria, na programu za ushauri kwa wanawake na wasichana walioko kwenye hali ya hatari. Kwa kushughulikia changamoto za mazingira na kijamii kwa pamoja, kikundi kinahakikisha kuwa matokeo ya kazi yao ni ya kina na endelevu.
“Tuligundua kuwa huwezi kumwezesha mwanamke bila kumpatia kwanza nafasi salama ya kusikilizwa, kupona, na kuanza maisha upya,” anasema Bi. Naiyan.
“Tree Nursery imetusaidia kutoka mbali kama vijana wa kike, kupitia hii kazi tunapata kitu kidogo nimefaidika sana na siwezi omba mtu kitu kwasbabu najua niko na kazi” anasema Mercy Chepukel, “wakati mwingine sisi wasichana tunapitia changamoto unapata unadhulumiwa, unalazimishwa uolewe na wengine wanapata mimba za mapema lakini kwa hapa (Paran women group) tumepata ,mafundisho ambayo imetusaidia sana kwamba una haki huwezi olewa mapema, uko na haki ya kusoma na ukidhulumiwa unaweza kuripoti na kupata haki”
Wakati wa ziara hiyo, nilivutiwa sana na hadithi ya mama mmoja aliyekuwa akifanya kazi katika bustani yake ya jikoni, jina lake ni Florence Chelelgo.
Kwa ujasiri mkubwa, Florence alinisimulia jinsi alivunja baadhi ya mila za zamani za jamii ya Maasai zilizowakandamiza wanawake na kuanza safari yake ya kujitambua kupitia Kikundi cha Wanawake cha Paran. “Sikuwa najua haki yangu hapa” alisema.
“Hapa masaini watu wanafinyilia sana wamama, wametufunza jinsi ya kutunza kitambulisho chetu,(National ID) kwasababu wazee walikuwa wanachukua wanaenda kuuza shamba” sahi tumewezeshwa tuko na mboga, machungwa, maembe na imetusaidia sana, sahi hatutegemei sana wazee wetu” alisema Florence.
Kupitia mafunzo na shughuli za uhifadhi wa mazingira, alipata maarifa, ujasiri, na nafasi ya kuwa kiongozi wa mabadiliko kijijini kwao Ololunga. Leo hii, Florence amejijengea uhuru wa kifedha kupitia miradi ya upandaji miti na ujasiriamali, akiendelea kuwahamasisha wasichana wadogo kutafuta elimu na ndoto zao.
“Baada ya kufika hapa (Paran) nimejua haki yangu kama Mama wa boma, kuanzia huo wakati maisha yangu yamebadilika. Hata mzee wangu alipoona nimekuja hapa na akaona vile nimebadilika najitafutia pesa kivyangu hata yeye akaanza kuacha ile mila ya kitambo ya Kimaasai” Anasema Florence. “tunahamasisha wanawake kujua haki zao na kuendelea kulinda mazingira.”
Hadithi yake inaakisi kiini cha mafanikio ya Paran Women Group: kuinua jamii kutoka ngazi ya msingi kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Mafanikio ya Kikundi cha Wanawake cha Paran yanatoa mafunzo ya thamani kwa jamii zingine kote nchini na hata kimataifa. Kazi yao inaonyesha kuwa suluhisho la changamoto za kimataifa linaweza kuanzia mashinani, na kuwawezesha wanawake ni njia ya uhakika ya kuleta mabadiliko chanya ya kudumu.
Katika wakati huu ambapo dunia inapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, juhudi kama hizi zinatukumbusha kuwa suluhisho endelevu inapatikana ndani ya ustahimilivu, ubunifu, na hekima ya jamii asilia. Kusaidia juhudi hizi si suala la huruma pekee bali ni hatua madhubuti kuelekea mustakabali jumuishi na endelevu kwa wote.
I am Versatile Multimedia Journalist with years of experience in Digital platforms, Live TV and Radio. In another world am a News Anchor and Reporter.