Kundi la wadukuzi la Anonymous laonya wabunge wa Kenya

Marion Bosire
2 Min Read

Kundi la kimataifa la wadukuzi wa mitandao ambalo pia ni la uanaharakati limetoa onyo kwa wabunge wa Kenya kuhusu mswada wa fedha wa mwaka 2024.

Wanachama wa kundi hilo walipachika ujumbe wa video kwenye akaunti yao rasmi ya mtandao wa X unaosema kwamba wamepata habari kuwa wabunge wa Kenya wanapanga kupitisha mswada wa fedha wa mwaka 2024 kinyume cha matakwa ya Wakenya.

“Tumepata taarifa kwamba mjadala unaendelea katika bunge la Kenya wa kupitisha mswada huo wa fedha ambao utasababisha Wakenya kutozwa kiwango cha juu cha ushuru,” wadukuzi hao walisema katika ujumbe wao.

Waliendelea kusema kwamba kwa bahati nzuri, nambari za simu za wabunge zimekuwa zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii na iwapo watakosa kusikiliza Wakenya na wapitishe mswada huo, basi siri zao zitatolewa kwa umma.

Kundi hilo linasema limeghadhibishwa na hatua ya maafisa wa usalama kuingilia maandamano ya amani yanayotekelezwa na Wakenya katika barabara za miji ya Nairobi na Mombasa.

Anonymous pia wanataka mswada huo utupiliwe mbali kabisa kama wanavyotaka Wakenya wengi.

Wakenya hasa wa umri mdogo walifanya maandamano ya amani jijini Nairobi juzi Jumanne kulalamikia mapendekezo yaliyo kwenye mswada wa fedha wa mwaka 2024 katika hatua ambayo imerejelewa tena leo Alhamisi.

Wabunge walianza kujadili mswada huo jana Jumatano na wanatarajiwa kukamilisha mjadala huo leo na kisha kuupigia kura mswada huo wiki ijayo.

Maafisa wa polisi wametumwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Nairobi kujaribu kuzima maandamano.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *