Kundi la Makoma larejea baada ya miaka 25

Waimbaji hao wametangaza tamasha kubwa ambalo wataanda Oktoba 24, 2025 jijini Paris, nchini Ufaransa.

Marion Bosire
2 Min Read

Kundi la muziki wa injili la Congo makoma limerejea baada ya miaka 20 ya ukimya, hali ambayo imefurahisha mashabiki wao.

Kupitia video ambazo wamekuwa wakichapisha kwenye mitandao ya kijamii, waimbaji hao wametangaza tamasha kubwa ambalo wataandaa Oktoba 24, 2025 jijini Paris, nchini Ufaransa.

Wanachama wa kundi hilo ambao ni wa familia moja wanafahamika kwa sauti zao za kipekee na utunzi wa hali ya juu wa nyimbo za mitindo ya pop na RnB.

Nyimbo zao ambazo waliimba kwa lugha za Lingala, kifaransa na kiingereza zilipendwa sana na wengi nchini Congo, Barani Afrika na hata nje.

Wanafamilia hao ambao sasa wanaishi nchini Uingereza ni pamoja na Annie Makoma, Pengani Makoma, Duma Makoma, Martin Makoma, Tutala Makoma na Patrick Badine.

Kundi hilo la Makoma liliteka anga za muziki mwisho mwisho wa miaka ya 1990 na mwanzo wa miaka ya 2000 kwa nyimbo kama Napesi, Butu na Moyi, Moto Oyo na Natamboli.

Wakati huo Makoma iliuza albamu zipatazo milioni 2, ikashinda tuzo mbali mbali kama za Kora katika kitengo cha kundi bora la muziki wa injili kati ya mafanikio mengine.

Baada ya kundi hilo kusambaratika mwaka 2004, Nathalie Makoma aliingilia uimbaji wa peke yake wengine wasijulikane walikokwenda.

Inasubiriwa kuona iwapo wamerekodi nyimbo mpya na iwapo zina mashiko kama nyimbo zao za awali.

Website |  + posts
Share This Article