Kundi la Ladysmith Black Mambazo latangaza kifo cha mmoja wao

Mazibuko alifariki jana Jumapili ya Pasaka akiwa amezingirwa na ndugu, jamaa na marafiki.

Marion Bosire
2 Min Read

Kundi la muziki la Ladysmith Black Mambazo limetangaza kifo cha mmoja wao aitwaye Albert Mazibuko kutokana na kile kilichotajwa kuwa kuugua kwa muda mfupi.

Mazibuko, mwanachama wa muda mrefu wa kundi hilo maarufu la muziki alifariki jana Jumapili ya Pasaka, na kifo chake kimetajwa kuwa pigo kubwa kwa bendi hiyo pamoja na jamii ya muziki duniani.

Kulingana na machapisho ya kundi hilo kwenye akaunti rasmi ya Facebook, Mazibuko aliaga dunia akiwa amezingirwa na ndugu jamaa na marafiki.

Mazibuko alijiunga na kundi hilo mwaka 1969 kwa mwaliko wa mwanzilishi Joseph Shabalala, na kuanza safari ya kipekee ya muziki iliyodumu kwa miaka 55.

Kwa zaidi ya miongo mitano, aligeuka kuwa nguzo muhimu ndani ya kundi, akijulikana kama “mkono wa kulia” wa Shabalala na baadaye kuwa mlezi na mshauri wa wanachama vijana baada ya mwanzilishi huyo kustaafu mwaka 2014.

Akijulikana kwa upole na unyenyekevu wake, Mazibuko aliheshimiwa sana kama balozi wa ujumbe wa kundi hilo wa amani, upendo na maelewano.

Alisafiri sana pamoja na kundi, akishirikisha muziki wao na urithi wa kitamaduni kwa hadhira kote duniani. Pia alikuwa sauti inayofahamika kwa vyombo vya habari, mara nyingi akiwakilisha kundi katika mahojiano na shughuli za umma.

Katika salamu zao za rambirambi, kundi hilo lilimwelezea kama “bora kuliko wote” na mtu ambaye wema wake uliwagusa wote aliokutana nao. Walionyesha huzuni kubwa, wakisema mioyo yao “imevunjika” kutokana na kifo chake.

Share This Article