Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Mutahi Kagwe, amewahakikishia wakulima kwamba kuna mbolea za kutosha katika ghala za Halmashauri ya Nafaka na Mazao nchini, NCPB.
Akiwahutubia wananchi katika soko la ESP eneo la Naromoru ,kaunti ya Nyeri, Kagwe alisema wizara yake imejizatiti kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo za kilimo za ubora wa hali juu na kwa bei nafuu.
Waziri huyo alidokeza kuwa katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la hitaji la mbolea ya bei nafuu, lakini serikali imekabiliana na hali hiyo kwa kuongeza kiwango cha mbolea katika ghala zote za NCPB kote nchini.
Kulingana na Kagwe, lengo la wizara yake ni kuhakikisha uzalishaji mazao unaongezeka maradufu ili taifa hili liwe na utoshelevu wa chakula, pamoja na kuwapiga jeki wakulima wadogo wadogo.
Aliyasema hayo jana Jumatatu alipoandamana na Rais William Ruto katika ziara ya Mlima Kenya, ambako viongozi hao walieleza umuhimu wa kuwa na masoko yatakayosaidia kuzuia hasara ya baada ya mavuno na kuimarisha kufanikisha wakulima na wateja kwa kuwawezesha wakulima kupata faida.