Uhalali wa jopo la majaji watatu walioteuliwa na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kusikiza kesi ya kupinga kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua utajulikana leo Jumatano alasiri.
Jopo hilo linajumisha majaji Eric Ogola anayeliongoza, Anthony Mrima na Freda Mugambi.
Mwilu aliliteua Jumamosi iliyopita, siku moja tu baada ya Mahakama ya Kerugoya kutoa agizo la kuzuia kuapishwa kwa Naibu Rais mteule Prof. Kithure Kindiki.
Ni hatua ambayo ilitifua kivumbi cha kisheria huku mawakili wa Gachagua wakipinga vikali kuteuliwa kwa jopo hilo.
Kulingana na mawakili hao wakiongozwa na Paul Muite, Naibu Jaji Mkuu hana mamlaka ya kuteua jopo hilo, na wajibu huo umetengewa Jaji Mkuu pekee.
Aidha, hawakufahamishwa kuhusiana na uteuzi huo na wanahoji ni kwa nini jopo hilo liliteuliwa mwishoni mwa wiki badala ya siku ya kazi ambayo ni Jumatatu hadi Ijumaa kama ilivyo kawaida.
Upande wa serikali ukiongozwa na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor unasema Naibu Jaji Mkuu ana mamlaka ya kuteua jopo hilo na wala hakufanya kosa lolote.
Upande huo unataka maagizo mawili yaliyotolewa yakizuia kuapishwa kwa Prof. Kindiki yafutiliwe mbali ili kupisha kuapishwa kwa mrithi huyo wa Gachagua ambaye alipigwa teke na Bunge la Seneti wiki jana.