KTDA kuelimisha umma kuhusu kilimo cha majani chai nchini

Martin Mwanje
2 Min Read
Afisa Mtendaji wa KTDA Wilson Muthaura (kulia) akimtuza mshindi wa shindano Davis Tamba 

Mamlaka ya Ukuzaji wa Majani Chai Nchini, KTDA imesisitiza dhamira yake ya kukuza uelewa wa umma kuhusiana na sekta ya majani chai na kuangazia wajibu muhimu unaotekelezwa na wakulima wadogo wadogo wa zao hilo katika sekta hiyo.  

Afisa Mtendaji wa KTDA Wilson Muthaura alielezea kuridhika kwake na wajibu unaotekelezwa na mamlaka hiyo katika kukuza mtagusano wa ubunifu na utamaduni kupitia mashindano ya uadishi wenye mandhari ya majai chai.

Muthaura aliyasema hayo wakati wa hafla ya utoaji tuzo kufuatia shindano la uandishi wa simulizi fupi iliyoandaliwa na Yours2read kwa ushirikiano na Chama cha Waandishi nchini Kenya.

Muthaura alielezea umuhimu wa shindano hilo katika kumulika simulizi za wakulima wa majani chai humu nchini.

“Tunajivunia kukuza mtagusano wa ubunifu na utamaduni kupitia mipango kama vile shindano la Yours2read la uandishi wenye mandhari ya majani chai. Mbali na kukuza hali ya kujielezea kifasihi, jitihada hii inaangazia simulizi za kuvutia za wakulima wa majani chai nchini Kenya,” alisema Muthaura.

Shindano hilo la mwezi mmoja lililenga kuongeza uelewa wa sekta ya majai chai wakati likikuza vipaji vya uandishi miongoni mwa washiriki.

Mshindi wa shindano hilo alikuwa Davis Tamba aliyetuzwa shilingi 30,000 huku Anene Anee akiibuka wa pili na kutuzwa shilingi 20,000.

Waliobuka wa tatu shindanoni ambao ni Nicholas Mokua, Abu Gee na Cynthia Dadia walituzwa na KTDA shilingi 10,000 kila mmoja.

Mkurugenzi Mkuu wa Yours2read Simon Norton alipongeza waliojitokeza kwa wingi kushiriki shindano hilo akisisitiza umuhimu wake katika kukuza ubunifu miongoni mwa washiriki.

 

Share This Article