KRA yazindua rasmi kituo cha utoaji huduma cha Malaba OSBP

Martin Mwanje
1 Min Read

Mamlaka ya Ukusanyaji Mapato nchini, KRA imezindua rasmi kituo cha utoaji huduma kutoka mahali pamoja cha Malaba OSBP katika eneo hilo la mpakani, kaunti ya Busia. 

Kituo hicho kinakusudia kuharakisha mchakato wa bidhaa zinazoruhusiwa kuingizwa nchini, kuboresha huduma za biashara na kuimarisha ukusanyaji mapato katika eneo hilo.

Kituo cha Malaba OSBP hushughulikia wastani wa malori 2,000 kwa siku huku malori 1,400 yakisafirisha bidhaa nje ya nchi kupitia kituo hicho na malori 600 yakiingiza bidhaa nchini.

Kulingana na KRA, idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na utekelezaji wa aina mpya ya utoaji huduma kwa wateja inayohakikisha huduma mbalimbali zinatolewa kutoka mahali pamoja.

“Kituo kipya cha utoaji huduma kinalenga kuboresha shughuli za mpakani na kusababisha kuimarika kwa mapato yanayokusanywa,” imesema KRA katika taarifa.

“Tangu kuzinduliwa kwa kituo cha Malaba OSBP, mapato yameongezeka kwa kiasi kikubwa huku kukiwa na ongezeko la asilimia 500 kutoka shilingi milioni 962 mwaka wa fedha wa 2012/2013 hadi shilingi bilioni 5.28 mwaka wa fedha 2023/2024.”

 

 

 

Website |  + posts
Share This Article