Maafisa kutoka Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA) wamenasa tani 52.5 za sukari ghushi katika kaunti ya Marsabit.
Sukari hiyo ilikuwa imepakiwa katika mifuko 2,100 ya kilo 25, ikiwa takriban wiki moja baada ya sukari nyingine kunaswa mjini Lodwar.
Maafisa wa KRA, wakishirikiana na polisi, walinasa sukari hiyo Novemba 4 ikisafirishwa na malori huku malori mengine mawili yakikamatwa siku moja baadaye katika duka moja mjini Marsabit yakijaribu kupakua sukari.
Sukari hiyo inaaminika kusafirishwa kutoka nchini Somalia na inakisiwa kuwa ya gharama ya shilingi milioni 6.41, kwa bei ya jumla na shilingi milioni 7.9 kwa bei ya rejareja.
KRA imesema ilipoteza ushuru wa kima cha shilingi milioni 10.14 kutokana na usafirishaji wa sukari hiyo ghushi.