Shirika la Ndege la Kenya Airways (KQ), limetangaza ushirikiano na msanii wa kimataifa Yemi Alade, ili kuimarisha soko lake la Afrika Magharibi.
KQ, imesema ushirikiano huo utaiwezesha kupata soko mpya Magharibi mwa Afrika, na kuimarisha uwepo wake katika eneo hilo.
“Tuko na fahari kutangaza ushirikiano wa kimkakati na msanii wa kimataifa Yemi Alande, ili kuimarisha uwepo wetu Afrika Magharibi,” ilisema KQ.
Afisa wa Kenya Airways anayesimamia biashara na wateja Julius Thairu, aliongoza hafla ya kutiwa saini kwa ushirikiano huo, akisema lengo kuu ni kufikia soko la Afrika Magharibi.
“Ushirikiano huu unajiri wakati ambapo unapanua uwepo wetu Magharibi mwa Afrika, hasaa baada ya kuongeza safari za ndege kuelekea na kutoka Lagos kwa ndege aina ya Boeing 787 Dreamliner, sasa ikiwa na safari sita kila wiki,” alisema Thairu.
Aidha, shirika hilo lilidokeza kuwa kupitia ushirikiano huo mashabiki wa Yemi Alade sasa watapata punguzo la asilimia 10 wanapotumia ndege za Kenya Airways kwa kutumia nambari KQXYEMI.