Wakulima wa Majani kutoka maeneo kadhaa ya ukuzaji zao hilo, wametoa wito kwa wabunge kuondoa ushuru wa asilimia 0.8 ambao umependekezwa kwenye Mswada wa Majani Chai.
Akizungumza katika kaunti ya Kiambu, mwenyekiti wa kiwanda cha Majani Chai cha Kagwe William Muroki Githumbi, alisema wakulima hawakuhusishwa kupitia kutoa maoni, na kutaja hatua hiyo kuwa kinyume cha katiba.
Githumbi alionya kuwa iwapo mswada huo ambao kwa sasa unasomwa mara ya pili bungeni utapitishwa jinsi ulivyo, utatoa fursa kwa baadhi ya mawakala kuchanganya Majani Chai ya kiwango cha chini na ile ya ubora wa juu kutoka kwa wakulima, hatua aliyotaja itawaathiri wakulima wanaokuza zao hilo la ubora wa hali ya juu.
Wakati huo huo mwenyekiti huyo aliwataka wabunge hasaa wanaotoka katika maeneo yanayokuza Majani Chai kuwaunga mkono wakulima na kulinda sekta hiyo dhidi ya kile alichokitaja kutozwa ushuru kupita kiasi.
Kulingana na mwenyekiti huyo, ushuru pamoja na matozo mengine kwenye Majani Chai, yameendelea kuongezeka na sasa yamefika asilimia 42.