Rais William Ruto amesema kuwa Hazina ya Miundombinu iliyobuniwa hivi karibuni itasaidia kupunguza bajeti, ushuru na madeni ya taifa.
Akizungumza leo Jumanne wakati wa uzinduzi wa uuzaji hisa za kampuni ya usafirishaji mafuta ya Kenya Pipeline, KPC katika soko la hisa la Nairobi, Ruto alisema hazina hiyo itafadhili miradi mikubwa ya miundombinu nchini.
Alisema uuzaji wa hisa za KPC umefanikisha kupatikana kwa shilingi bilioni 106 ambazo zitawekezwa ili kupata shilingi trilioni 1.2.
“Hivi ndivyo tutakavyobadilisha taifa hili,” alisema Rais Ruto.
Aliwahakikishia Wakenya kuwa mapato yanayotokana na uuzaji wa hisa za kampuni ya Kenya Pipeline, yatatumiwa kwa ustawi wa miundombinu, na kwamba fedha hizo hazitaelekezwa kwa ulipaji madeni na mishahara.
Aidha, alidokeza kuwa ubinafsishaji umesaidia kuimarisha thamani ya mali ya umma ambayo tayari imekomaa.