KQ na Jambo Jet zafutilia mbali safari za ndege

Tom Mathinji
1 Min Read
Ndege ya shirika la Kenya Airways.

Shirika la ndege la Kenya Airways, KQ na kampuni ya Jambo Jet zimetangaza kufutilia mbali safari zao za ndege, kufuatia mgomo unaoendelea wa wafanyakazi wa safari za ndege kote nchini.

Mgomo huo ulioanza Jumanne usiku, unaongozwa na chama cha wafanyakazi wa safari za ndege, KAWU, kupinga hatua ya serikali ya taifa ya kukodisha shughuli za viwanja vya ndege kwa kampuni ya Adani holdings, yenye makao yake nchini India.

“Tunaendelea kukadiria hali ilivyo, na tutawafahamisha kuhusu safari zilizoathiriwa,” ilisema KQ kupitia taarifa fupi.

Kwa upande wake, kampuni ya Jambo Jet, iliwataka wateja wake kutoelekea katika uwanja wa ndege, hadi watakapofahamishwa kufanya hivyo.

“Tunawashauri msielekee katika viwanja vya ndege, hadi tutakapowafahamisha kuhusu ratiba mpya,” ilisema kampuni ya Jambo jet katika taarifa kwenye ukurasa wake wa X.

Katibu Mkuu wa chama cha wafanyakazi wa safari za ndege KAWU, Moss Ndiema, aliitaka serikali kubatilisha hatua ya kuikabidhi kampuni ya Adani usimamizi wa viwanja vya ndege hapa nchini

Wasafiri katika viwanja vya ndege kote nchini walitatizika kutokana na mgomo huo.

TAGGED:
Share This Article