Watu wanne wamefariki kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea katika eneo la Katakala huko Narok Kusini.
Ajali hiyo ilihusisha trela na gari la kubeba watalii aina ya Toyota Landcruiser linalomilikiwa na kampuni ya Dallok Magnifiers Tours Safaris.
Watatu kati ya wanne waliofariki wanasemekana kuwa watalii ambao ni raia wa kigeni na mwingine ni dereva aliyekuwa akiendesha gari walimokuwa wakisafiria.
Dereva wa trela alinusurika ila na majeraha miguuni.
Ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa gari la watalii kutaka kuipita trela hiyo visivyotakikana na kusababisha gari hilo kugongana na trela hiyo iliyokuwa ikitokea upande mwingine.
Miili ya waliofariki imepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya kaunti ya Narok huku magari yote mawili yakikokotwa hadi kituo cha polisi cha Narok ili kufanyiwa ukaguzi.
Hayo yanajiri huku ajali nyingine mbaya ikiripotiwa kutokea kwenye barabara kuu ya kutokea Eldoret hadi Nakuru.
Ajali hiyo ilihusisha basi la shule ya Rockside Academy Utawala lililokuwa likitoka kwenye tamasha la kitaifa la muziki mjini Eldoret likielekea Nairobi. Lilikuwa limebeba wanafunzi 26, walimu watatu na mpishi mmoja.
Basi hilo liligongwa na winchi baada ya dereva wa winchi hiyo kushindwa kuidhibiti.
Majeruhi walikimbizwa katika hospitali mbalimbali mjini Molo ili kupata matibabu.