Mamlaka inayosimamia bandari nchini KPA imeelezea kwamba kuna uwezekano kwamba hitilafu ya umeme ndiyo ilisababisha mlipuko kwenye meli ya mafuta iliyokuwa imetia nanga katika kituo cha African Marine huko Liwatoni jana alasiri.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari KPA ilielezea kwamba meli hiyo ilikuwa imetia nanga karibu na kituo cha kibinafsi cha kukarabati meli cha kampuni ya African Marine General Engineeringkisa hicho kilipotokea.
Mashua ya KPA kwa jina Simba III ambayo ina vifaa vya kuzima moto ilisaidia kuuzima kunako saa moja baada ya kisa hicho kuripotiwa.
Kulingana na taarifa ya KPA, hatua za haraka zilizochukuliwa na wafanyakazi wa dharura kwenye Simba III na wazima moto zilisaidia kurejesha utulivu katika eneo hilo.
Mlipuko huo hata hivyo ulisababishia mhudumu mmoja wa meli majeraha madogo na alikimbizwa hospitali ambapo anaendelea kupata nafuu.
Mkurugenzi mtendaji wa KPA William Ruto alipongeza kikosi hicho cha mashua ya huduma za bandarini ya Simba III kwa kuweza kuzima moto huo.