Mahakama imetoa kibali cha kukamatwa kwa walinzi 10 wa baa ya Kettle House & Grill waliokosa kufika mahakamani kuhusiana na kushambuliwa kwa waandishi wa habari na maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi Mabaya ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA) siku chache zilizopita.
Maafisa hao pamoja na waandishi wa habari, wakiwemo wa shirika la utangazaji nchini, KBC walishambuliwa walipofika iliko baa hiyo mtaani Lavington jijini Nairobi kufanya msako dhidi ya wavutaji wa shisha.
Matumizi ya bidhaa hiyo yamepigwa marufuku nchini Kenya kwa kipindi cha miaka 7 sasa.
Walinzi 11 wanaoshukiwa kuhusika katika ushambuliaji huo walifikishwa mahakamani leo Jumatano.
Walikanusha mashtaka dhidi yao na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu 30 pesa taslimu au dhamana ya shilingi laki moja.
Mshukiwa wa uuzaji wa shisha aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu 10 pesa taslimu.
Hakimu Mkuu Gilbert Shikwe alitoa kibali cha kukamatwa kwa walinzi 10 waliokosa kufika mahakamani leo Jumatano kukabiliana na mashtaka dhidi yao.
Kesi hiyo itasikizwa Januari 24, 2024.