Korea Kaskazini yalaani mpango wa Amerika wa kutuma nyambizi za kivita hadi pwani ya Korea

Marion Bosire
3 Min Read

Korea Kaskazini imelaani mpango wa Amerika wa kutuma nyambizi zilizo na zana za kunuklia na makombora karibu na sehemu ya Korea inayozungukwa na maji mengi ikionya kwamba hatua hiyo huenda ikazusha mzozo mbaya wa atomiki.

Taarifa ya msemaji mmoja wa wizara ya ulinzi ya Korea Kaskazini iliyochapishwa na shirika la habari la Korean Central News Agency – KCNA inasema mpango huo wa Amerika ulioafikiwa na viongozi wa Amerika na Korea Kusini mwezi Aprili una uwezo wa kusafirisha zana za ki-nuclear za Amerika hadi pwani hiyo ya Korea kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1981.

Msemaji huyo aliendelea kusema kwamba ni hali hatari kwa sababu itasababisha mvutano wa kijeshi katika kanda hiyo na kusababisha mzozombaya zaidi wa ki- nuclear. Kulingana naye, mpango wa Amerika ni usaliti wa ki-nuclear dhidi ya Korea Kaskazini na nchi jirani na unatishia usalama.

Rais wa Amerika Joe Biden na mwenzake wa Korea Kusini, Yoon Suk-yeol, walikubaliana mjini Washington mwezi Aprili kwamba nyambizi ya America yenye zana za ki-nuclear na kombora ingezuru Korea Kusini, lakini hawakutoa tarehe kamili ya ziara hiyo.

Ziara hiyo inanuiwa kutuma zana za Amerika ili kuweza kujibu mipango inayozidi kuongezeka ya Korea Kaskazini ya zana za ki-nuclear na makombora.

Mwezi jana nyambizi ya kivita ya Amerika iliwasili kwenye bandari ya Busan huko Korea Kusini na awali ndege ya kivita ya Amerika yenye uwezo wa kurusha mabomu ilikuwa imetumika katika mafunzo na matayarisho ndani ya Korea Kusini katika onyesho la nguvu kufuatia kutibuka kwa mpango wa Korea Kaskazini wa kuzindua satellite ya kijasusi.

Korea kaskazini inadai pia kwamba hivi maajuzi ndege za kijasusi za jeshi la Amerika ziliingia bila idhini kwenye anga yake karibu na pwani ya mashariki.

Taarifa hiyo ya msemaji wa wizara ya ulinzi ya Korea Kaskazini ambaye hakutajwa iligusia visa vya awali ambapo nchi hiyo ilidungua au kukatiza safari za ndege za Amerika katika mpaka wake na Korea Kusini.

Vitisho hivi vya Korea Kaskazini vinajiri wakati kiongozi wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol, anajiandaa kuhudhuria mkutano wa shirika la kujihami la NATO mjini Vilnius, nchini Lithuania Jumanne na Jumatano.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *