Inspekta Mkuu wa Polisi Japhet Koome amepuuzilia mbali madai kuwa polisi kadhaa kutoka Kenya wameuawa nchini Haiti.
Tayari kundi la maafisa 400 wa polisi wameelekea katika nchi hiyo ya Carribean ambayo inakumbwa na changamoto za magenge ya wahalifu ili kusaidia katika juhudi za kudumisha usalama nchini humo.
“Nadhari ya ofisi hii imeelekezwa madai yasiyokuwa na msingi, ya uongo, yasiyokuwa ya kizalendo na yenye nia mbaya yanayosambaa katika mitandao ya kijamii yakiashiria kwamba maafisa saba wa Huduma ya Taifa ya Polisi wameuawa nchini Haiti,” alisema Koome katika taarifa ya ukurasa mmoja leo Jumatatu.
“Tungependa kubainisha kwa umma kuwa maafisa wetu waliondoka nchini Kenya Juni 24, 2024 na si tu kwamba walipokelewa vyema na raia Haiti punde baada ya kuwasili, lakini wote wako salama na tayari kutekeleza majukumu yao bayana na mahususi.”
Kulingana na Koome, tangu walipowasili nchini Haiti, maafisa hao wamekuwa wakifanya kazi na Polisi wa Taifa wa Haiti na hadi kufikia sasa, wamekuwa wakichunguza maeneo muhimu ambayo ni changamoto kufanya operesheni. Aidha, ameashiria kuwa mara kadhaa wameshirika doria kwa pamoja ndani ya mji wa Port-au-Prince.