Kongamano la vyama vya akiba na mikopo Afrika kuandaliwa Oktoba Botswana

Marion Bosire
2 Min Read

Shirikisho la Vyama vya Ushirika, Akiba na Mikopo barani Afrika, ACCOSCA litaandaa awamu ya 23 ya kongamano la kila mwaka la vyama hivyo, Oktoba 8 hadi 13 jijini Gaborone nchini Botswana.

Wahusika kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni watakusanyika kuangazia mikakati na ubunifu wa kuhakikisha ustawi wa vyama hivyo vya kifedha.

Kulingana na takwimu za makongamano ya awali, wajumbe wapatao 1,000 wanatizamiwa kuhudhuria kongamano la mwaka huu.

Waziri wa Maendeleo ya Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo na za Kadiri nchini Kenya Simon Kiprono Chelugui, aliandaa mkutano wa wadau kujiandaa kwa kongamano hilo lijalo.

Dhamira ni kuhakikisha wawakilishi wanadhihirisha kujitolea kwa Kenya kupiga jeki vyama vya ushirika, akiba na mikopo ili vikue na kuchangia maendeleo ya kijamii.

Mkutano huo wa leo asubuhi ulilenga pia kutathmini mialiko ya kongamano lijalo la Afrika, maandalizi ya maonyesho na hotuba zinazotarajiwa kutokana na kongamano hilo na maandalizi ya Kenya kuandaa awamu ya 24 ya kongamano la bara Afrika la vyama vya ushirika, akiba na mikopo mwaka ujao wa 2024.

Wadau wa sekta hiyo waliangazia pia umuhimu wa Wakenya kuhudhuria kongamano la Botswana huku viongozi wa mashirika ya akiba na mikopo nchini wakihimizwa kuhudhuria.

Katika kongamano la mwaka huu nchini Botswana, Kenya itapokezwa bendera ya maandalizi.

Share This Article