Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC pamoja na wa masuala ya jumuiya hiyo wanakamilisha kongamano lao kisiwani Zanzibar leo Jumatatu ambapo wamekuwa tangu Jumamosi Julai 6, 2024.
Lengo kuu la kongamano hilo la Julai 6 hadi 8 Julai, 2024 ni kujadiliana kuhusu amani na usalama na masuala mengine muhimu yanayohusu eneo la Afrika Mashariki.
Kongamano hilo ni utekelezaji wa maelekezo yaliyoafikiwa kwenye mkutano wa mawaziri wa EAC Januari 16, 2024 jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia.
Wakati wa mkutano huo, Mawaziri wa Mambo ya Nje na wa masuala ya EAC walikubaliana kwamba ipo haja ya kuandaa kongamano la kujadili kwa kina vikwazo vya uwianishaji wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Katibu Mkuu wa EAC Veronica Nduva alitaja kongamano linaloendelea kama jukwaa la mazungumzo wazi, mipango ya kimkakati na utambuzi wa hatua zinazofaa kuchukuliwa ili kuimarisha amani na usalama huku zikistawisha na kukuza mipango ya kuwianisha eneo zima la EAC.
Waziri wa Mambo ya Nje na ya EAC nchini Tanzania January Makamba, ambaye ni mwenyeji wa wenzake kwenye kongamano hilo alisisitiza umuhimu wa umoja kati ya nchi wanachama wa EAC akisema ni kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi na Penina Malonza ambaye ni Wwaziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Maeneo Kame, wanawakilisha Kenya katika kongamano hilo.