Kongamano la pili la kimataifa la uwekezaji la kaunti ya Homa Bay litaanza kesho, Februari 27, 2024.
Lengo kuu la mkutano huo wa siku tatu utakaokamilika Februari 29, 2024, ni kuvutia wawekezaji wa humu nchini na wale wa kimataifa kutumia fursa zilizopo za uwekezaji katika kaunti hiyo.
Akizungumza wakati wa mkutano wa maandalizi ya kongamano hilo mjini Homa Bay, Naibu Gavana wa kaunti hiyo Joseph Oyugi Magwanga aliwatia moyo wawekezaji kutoa kipaumbele kwa utoaji wa nafasi za ajira kwa wakazi.
Magwanga anaamini hatua hiyo itasaidia kupunguza pakubwa visa vya uhalifu katika eneo hilo, akiongeza kusema kwamba kaunti ya Homa Bay ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya utalii hasa katika fuo za Ziwa Viktoria.
Waziri wa Utalii na Uwekezaji wa kaunti ya Homa Bay Polycarp Okombo alifichua mipango ya kongamano la kesho alilosema huenda likahudhuriwa na mabalozi wa Marekani na Poland.
Okombo alisema wameangazia pakubwa kilimo biashara hasa uzalishaji wa mafuta ya kupikia kama vile mafuta ya mawese na wanataka kutumia ipasavyo uwezo wa kaunti hiyo kupitia fursa hii.
Aguko Juma, mkulima na ambaye aliwahi kuhudumu kwenye serikali ya kaunti, alitaja faida iliyoko katika kilimo biashara huku akihimiza wengine kuwekeza katika sekta hiyo.
Mikataba ya maelewano inatarajiwa kutiwa saini kati ya serikali ya kaunti ya Homa Bay na wawekezaji au kati ya wawekezaji wakati wa kongamano hilo.
Kaunti ya Homa Bay ambayo ina sehemu kubwa ya Ziwa Viktoria inatizamia ongezeko la shughuli za utalii punde baada ya fursa za uwekezaji katika sekta hiyo kugunduliwa.
Mandhari ya awamu ya pili ya kongamano la uwekezaji la Homa Bay ni “Kufungua Ghuba yenye Uwezo Usiokuwa na Mwisho” yaani “Unlocking the Bay of Endless Potential”.
Waandalizi wanalenga kuvutia washiriki wapatao elfu 2 wa mashirika mbalimbali yakiwemo yale ya serikali kuu, wawekezaji wa kitaasisi, wawekezaji wa kibinafsi, serikali za kaunti, taasisi za elimu kati ya wengine.
Awamu ya kwanza ya kongamano la uwekezaji la Homa Bay iliandaliwa Februari 18 na 19 mwaka 2016 katika hoteli ya Tourist na Gavana wa wakati huo Cyprian Awiti.