Mudavadi asisitiza umuhimu wa ushirikiano kuchochea maendeleo

Martin Mwanje
2 Min Read

Kinara wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi ametoa wito wa uboreshaji wa ushirikiano kati ya Canada na nchi za bara la Afrika ili kutumia wingi wa rasilimali zilizomo barani humo kufikia maendeleo endelevu kwa manufaa ya raia. 

Mudavadi amesema Afrika ina rasilimali nyingi za madini, nishati mbadala na mashamba mengi ya kilimo na hivyo kulifanya bara hilo kuwa eneo bora la maendeleo endelevu.

“Hebu tutafute nyanja mpya ili tuwe na uwekezaji mbalimbali wa bidhaa tunazouza nje ya nchi katika nyanja kama vile kilimo endelevu na nishati safi, na kuhakikisha kuwa ushirikiano huu muhimu unachangia ustawi wa pamoja,” alisema Mudavadi leo Jumatatu asubuhi katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa Biashara kati ya Afrika na Canada jijini Nairobi.

“Ningependa kutoa wito kwa kampuni zetu kutumia fursa hii kukuza ushirikiano, kuanzisha ushirikiano, na kutafakari juu ya fursa nyingi zilizopo mbele. Tunaporejelea safari hii pamoja, hebu tukumbatie ari ya ushirikiano. Hebu tufanye kazi bega kwa bega na kuzishinda changamoto zetu na kujenga siku bora za usoni kwa ajili ya vizazi vijavyo.”

Mkutano wa Biashara kati ya Afrika na Canada unachukuliwa kuwa hatua kubwa katika kuimarisha uhusiano wa biashara kati ya mataifa na kutafuta fursa mpya za ushirikiano.

 

Website |  + posts
Share This Article