Koffi Olomide kuandaa tamasha nchini Kenya

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki tajika kutoka nchini Congo Antoine Christophe Agbepa Mumba, maarufu kama Koffi Olomide anatarajiwa kutumbuiza nchini Kenya kwa mara ya kwanza tangu alipotimuliwa nchini mwaka 2016.

Kupitia mitandao ya kijamii, Koffi alitangaza kwamba ataandaa tamasha nchini Kenya Disemba 8 na 9 2023, katika ukumbi wa uwanja wa michezo wa Kasarani.

Alitoa mwaliko kwa wote ambao wanapenda muziki wake wajumuike naye siku hizo mbili huku akiahidi burudani ya hali ya juu.

Kisa cha mwaka 2016 kilisababisha atimuliwe nchini kutokana na lalama za wengi mitandaoni hasa kina dada.

Alionekana kwenye video akimpiga teke tumboni mmoja wa wacheza densi wake katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta muda mfupi baada ya kuwasili.

Baadaye jioni siku hiyo maafisa wa polisi walimkamata nje ya afisi za kampuni moja ya vyombo vya habari baada ya kuhojiwa kuhusu tamasha yake ambayo mwishowe haikufanyika.

Siku iliyofuata, Koffi alipandishwa ndege kuelekea jijini Kinshasa nchi Congo.

Mwaka 2020 Koffi aliomba msamaha kutokana na kisa hicho ambacho kilimharibia uhusiano na watu wa Kenya na hata serikali. Alikuwa amepitia Kenya akielekea nchini Tanzania kwa tamasha na kurekodi muziki na wasanii wa huko.

TAGGED:
Share This Article