KNUT yafutilia mbali mgomo, KUPPET yasimama kidete kuendelea na mgomo

Dismas Otuke
2 Min Read

Muungano wa vyama vya walimu wa shule za msingi nchini KNUT,umefutilia mbali mgomo wa kitaifa uliokuwa uanze leo usiku wa manane, huku wenzao wa KUPPET wakiapa kugoma Jumatatu.

Baraza kuu la KNUT kupitia kwa Katibu Mkuu Henry Oyuu, limetoa taarifa kwa vyombo vya habari Jumapili jioni kutangaza kusitishwa kwa mgomo huo wa kitaifa.

Hii inafuatia mazungumzo yaliayoandaliwa kati ya walimu  na tume ya kuwaajiri walimu nchini TSC Agosti 19 ambapo maswala tata yalijadiliwa kwa kina .

Maswala yaliyoibua utata yalikuwa ni utekelezeaji kikamilifu kwa nyongeza ya mshahara wa mwaka 2021/2025 ambapo TSC tayari imetekeleza katika mishahara ya mwezi Agosti,kupandishwa vyeo kwa walimu huku TSC, ikithibitisha kuwa tayari walimu 51,232 kati ya 78,768 wamepandishwa vyeo.

Mgomo uliokuwa umeitishwa na KNUT ulikuwa unatishia kudumaza masomo na mitahani ya kitaifa kwa shule za msingi katika muhula wa tatu.

Hata hivyo upande wa pili wa sarafu Chama cha walimu wa shule za sekondari na vyuo KUPPET kimesimama kidete kuwa mgomo wake ungalipo na kuwataka walimu kote nchini kutoripoti shuleni kesho.

Kwenye mahojiano ya kipekee kwa njia ya simu na Katibu Mkuu wa KUPPET Akelo Misori ,mgomo wao ungalipo ilivyopangwa baada ya TSC kukosa kutimiza matakwa yao.

“Sisi mgomo wetu ungalipo tulivyopanga na walimu wetu hawataripoti shuleni kesho kwa muhula wa tatu,hadi serikali itakapoangazia kikamilifu matakwa yetu yote.”amesema Misori

Shule koote nchini zitafunguliwa kwa muhula wa tatu na wa mwisho Jumatatu Agosti 26 huku mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE ikitarajiwa kung’oa nanga mwezi Oktoba.

Website |  + posts
Share This Article