Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta – KNH imefanikiwa kufanya upasuaji wa kwanza wa aina yake duniani wa kurejesha sura ya mtoto aliyejeruhiwa vibaya usoni kutokana na shambulio la majambazi.
Upasuaji huo wa saa tisa ulifanyika Alhamisi, Septemba 25, 2025 na ulitekelezwa na kundi la wataalamu wa fani mbalimbali kutoka KNH na Chuo Kikuu cha Nairobi – UoN, ukilenga kurejesha sura ya mvulana huyo aliyepigwa risasi Desemba 23, 2023.
Tukio hili linaweka rekodi ya kimataifa na kuipa Kenya nafasi ya kipekee katika medani ya upasuaji wa hali ya juu na uvumbuzi wa kiteknolojia ya tiba.
Upasuaji huo ulijumuisha urejeshaji mgumu na wa kina wa maeneo ya usoni ili kurudisha sura na utendaji kazi wa maeneo yaliyoharibiwa na ndio wa kwanza wa aina hiyo duniani.
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa KNH, Dkt. Richard Lesiyampe, aliisifu timu ya madaktari kwa ujuzi wao wa hali ya juu, kujitolea na ujasiri waliouonesha.
“Tukio hili ni ushahidi wa ujuzi na dhamira ya madaktari wetu, na pia linaonesha uongozi wa Kenya unaoimarika katika huduma maalumu za afya. Ni ujumbe wa matumaini kwa wagonjwa kote Afrika na duniani,” alisema Dkt. Lesiyampe.
Mtoto huyo, Ian Baraka mwenye umri wa miaka 7, kwa sasa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na anaendelea kupokea uangalizi wa karibu wa kitabibu.
Ian alipata majeraha mabaya ya usoni tarehe 23 Desemba 2023, katika mpaka wa Isiolo na Meru, aliposhambuliwa na risasi ya majambazi waliovamia kijiji chao. Tangu hapo, amekuwa akipokea matibabu ya kina na hatua za urekebishaji kutokana na majeraha aliyoyapata kwenye macho na taya la chini.
Upasuaji huu wa kipekee uliongozwa na timu maalum ikiwemo Prof. Symon Guthua (Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Meno na Uso), Dkt. Margaret Mwasha (Mshauri Bingwa wa Urekebishaji wa Sura – Prosthodontist), na Dkt. Andrew Okiriamu (Daktari wa Upasuaji wa Meno na Uso).
Shukrani maalum zimetolewa pia kwa Dkt. Branice Munyasha, mwanafunzi wa upasuaji wa uso na taya (Maxillofacial Surgery), ambaye alikimbia marathoni mbili ili kuchangisha fedha kwa ajili ya upasuaji wa Ian.
Uongozi wa hospitali umeahidi kuendelea kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya Ian kwa wakati ufaao, huku wakiheshimu faragha na ustawi wa familia yake.