Baraza la Mitihani Nchini, KNEC na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu wameshtakiwa mahakamani na wazazi wa mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi ya Set Greenhills Academy Kisii kuhusiana na matokeo ya mtihani.
Matokeo hayo ya mtihani wa darasa la 8, KCPE ya mwaka 2023 yalitangazwa na Waziri Machogu Alhamisi wiki iliyopita.
Katika kesi hiyo, wazazi hao waliomba mahakama isimamishe mchakato wa uteuzi wa wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza unaofaa kuanza kesho ili kutoa muda wa kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi hiyo.
Kulingana nao, mwanao anasema karatasi zake za mtihani hazikusahihishwa ipasavyo na alama alizopatiwa sio zake na hilo limemsababishia msongo wa mawazo.
Wanaonelea kwamba iwapo mchakato huo wa uteuzi utaendelea, muda uliotolewa wa kuhakiki majibu ya wanafunzi kadhaa waliolalamika hautakuwa na maana kwani huenda mwanao na wengine wakakosa nafasi katika shule ambazo wangependelea.
Awali, KNEC ilikiri kwamba kulikuwa na makosa katika matokeo ya wanafunzi kadhaa nchini.
Wazazi wa shule ya Kitengela International pia wamechukua hatua sawia ya kuelekea mahakamani kutafuta haki kwa wanao.