KMTC yafungua tovuti kwa ajili ya usajili wa wanafunzi wapya wa mwezi Machi

Marion Bosire
2 Min Read
Katibu katika wizara ya afya, Mary Muthoni.

Taasisi ya mafunzo ya utabibu nchini KMTC imetangaza ufunguzi wa tovuti yake kwa ajili ya usajili wa wanafunzi wapya wa taasisi hiyo ambao watajiunga rasmi mwezi Machi mwaka huu.

Kupitia taarifa idara ya serikali ya afya ya umma na viwango vya utaalamu imesema kwamba maombi ya kujiunga na taasisi hiyo kwa ajili ya kozi za vyeti na stashahada yanatumwa kupitia kwa tovuti ya taasisi inayohusika na usajili wa wanafunzi kwenye vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu nchini KUCCPS.

KUCCPS ilikuwa imetangaza kuongezwa kwa muda wa kutuma maombi ya kujiunga na taasisi mbali mbali hadi Machi 4, 2024 na hivyo fursa za KMTC za stashahada na vyeti ziko wazi hadi tarehe hiyo.

Usajili wa wahudumu wa afya ambao wangependa kuongeza masomo unatekelezwa kupitia tovuti ya KMTC ambayo ni admissions.kmtc.ac.ke shughuli ambayo itaendelea hadi idadi hitajika ya wanafunzi itakapoafikiwa katika kila kozi.

Hata hivyo usimamizi wa taasisi hiyo unadhamiria kupokea wanafunzi wa kozi hizo kufikia Machi 12, 2024 tayari kuanza masomo.

Katibu katika idara ya afya ya umma Mary Muthoni ambaye alitia saini taarifa hiyo alisema kwamba wanasubiri kwa hamu kubwa kukaribisha wanafunzi wapya katika taasisi ya KMTC.

Watakaokumbana na matatizo katika kutuma maombi ya kujiunga na taasisi ya KMTC wameshauriwa kuwasiliana na usimamizi kupitia nambari za simu 0736993813, 0736212060, 0723000429 au 0723004516.

Wanaweza pia kutuma barua pepe kwa anwani admissions@kmtc.ac.ke

Share This Article