Chama cha Madaktari nchini, KMPDU, kimetangaza kushiriki maandamano leo Jumanne, kulalamikia kudorora kwa mfumo wa afya hapa nchini.
Kupitia kwa ilani iliyotumwa kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt. Davji Atellah alithibitisha kuwa maandamano hayo yataandaliwa baada ya kuwahutubia wanahabari katika hospitali kitaifa ya Kenyatta.
Maandamano hayo yanatarajiwa kupitia katika Wizara ya Afya, Tume ya Kuratibu Mishahara na Marupurupu, SRC na katika Hazina Kuu.
Chama hicho kinaitaka serikali kushughulikia maswala muhimu ya afya, yakiwemo maslahi ya wahudumu wa afya na kutatua changamoto zilizoibuliwa za uajiri.
KMPDU, imekuwa ikiangazia changamoto zinazowakumba wahudumu wa afya, ikiwa ni pamoja na kucheleweshwa kwa mishahara, ukosefu wa vifaa vya matibabu, na serikali kukosa kutimiza masharti kadhaa ya kazini.