Kituo kipya cha huduma chafunguliwa Nanyuki

Marion Bosire
2 Min Read

Naibu rais Rigathi Gachagua amezindua kituo kipya cha huduma katika eneo la Makutano kaunti ndogo ya Laikipia Mashariki.

Akizungumza siku ya Jumatatu baada ya uzinduzi huo, naibu rais alisema kuwa kituo hicho cha kisasa kitaleta afueni kwa wakazi kwa kuwa hawatasafiri zaidi ya kilomita 78 tena wakitafuta huduma za serikali katika kaunti za Nyeri na Nyandarua.

Alisema kuwa ujenzi wa kituo hicho cha Makutano uliharakishwa kwa sababu kuu ya wakazi kuhitaji huduma za serikali na pia kwa azma ya serikali ya kuwapa huduma wananchi.

“Kwa kituo hiki cha 51, tunasambaza huduma zinazozingatia watu nyanjani. Tunafikia zaidi ya wateja 60,000 kwa siku kupitia vituo vya Huduma katika kaunti 33 kote nchini,” alisema Gachagua.

Gachagua alitoa wito kwa serikali ya kaunti kutoa kipaumbele kwa mambo ya kidijitali kwa kuweka huduma zake kwenye mtandao ili kurahisisha huduma kwa Wakenya na kupunguza ufisadi wakitafuta huduma za serikali.

“Katika miaka 10 iliyopita, vituo vya Huduma vimethibitisha kuwa sehemu muhimu sio tu katika utoaji wa huduma bali pia mfumo wa usaidizi wa ajira na ni kwa sababu hii, kwamba serikali inajitahidi kuanzisha vituo hivyo katika maeneo bunge 290,” alifichua naibu rais.

Kituo hicho cha kisasa kilijengwa kwa ufadhili wa hazina ya ustawi wa maeneo bunge (NG-CDF) kwa gharama ya shilingi milioni 52.

Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri aliwataka viongozi wa eneo hilo kutosusia miradi ya serikali iliyoanzishwa na watangulizi wao inayolenga kunufaisha wakazi.

Viongozi walioandamana na naibu rais ni gavana wa Laikipia Joshua Irungu, gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, mbunge wa Laikipia Magharibi Wachira Karani na mwakilishi wa kike wa kaunti ya Laikipia Jane Kagiri miongoni mwa wengine.

Share This Article