Kituo cha utamaduni wa Msumbiji na China kuzinduliwa Maputo

Marion Bosire
2 Min Read
Rais Filipe Nyusi

Rais wa Msumbiji Filipe Jacinto Nyusi ameagiza kwamba uzinduzi wa kituo cha ushirikiano wa kitamaduni kati ya China na Msumbiji uandaliwe kwa pamoja na sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Samora Moisés Machel.

Hafla hiyo inapangiwa kuandaliwa Septemba 28, 2023 katika bewa kuu la Chuo Kikuu cha Eduardo Mondlane, jijini Maputo. Angekuwa hai, Machel angekuwa anatimiza umri wa miaka 90.

Kituo hicho cha utamaduni ambacho kilibuniwa kutokana na uhusiano mzuri ulioko kati ya China na Msumbiji ndicho cha pili kwa ukubwa barani Afrika. Kimejengwa kwenye ardhi ya mita elfu 20 mraba.

Kinasheheni kumbi nyingi za maonyesho, vyumba vya kuandaa mikutano, ukumbi mkubwa wenye nafasi ya watu 1500, studio kadhaa pamoja na vyumba vya wanamuziki na waigizaji kujiandaa kwa maonyesho. Vipo pia vyumba vya kuonyesha kazi za sanaa na bidhaa nyingine.

Kituo hicho kinadhamiriwa kuchangia pakubwa katika matangazo na maendeleo ya maonyesho ya kitamaduni nchini Msumbiji na hata nje.

Kitatoa pia nafasi za ajira na kuwa chanzo cha mapato kwa wahudumu na wasanii mbali na kufanya jiji la Maputo kuvutia watalii na wanabiashara.

Baada ya kuzinduliwa rasmi, kutaandaliwa maonyesho katika kituo hicho kati ya Septemba 28 na 30.

Balozi wa China nchini Msumbiji Wang Hejun alitangaza kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho cha utamaduni jijini Maputo mwaka jana.

Viongozi wa serikali ya kitaifa, serikali za mikoa, mabalozi na wananchi kwa jumla wamealikwa kuhudhuria sherehe hizo.

Share This Article