Kituo cha utafiti wa sayansi ya michezo chazinduliwa

Marion Bosire
2 Min Read

Serikali imezindua kituo cha utafiti wa sayansi ya michezo cha Shirika la Utafiti wa Kimatibabu Nchini, KEMRI mjini Eldoret katika juhudi za kukabiliana na tatizo linalozidi kuongezeka la matumizi ya dawa za kusisimua misuli miongoni mwa wanariadha.

Kituo hicho ambacho ni cha 15 cha KEMRI kinalenga pia kupanua utafiti wa afya katika michezo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kituo hicho leo Alhamisi, Waziri wa Afya Susan Nakhumicha alitambua umuhimu wake katika kufanikisha utafiti dhidi ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli ambayo ni tishio kubwa kwa mafanikio ya nchi hii katika riadha.

Alisema changamoto zinazokabili Kenya inapotafuta kukabiliana na matumizi ya dawa hizo ni nyingi ikiwemo ukosefu wa maabara iyoidhinishwa ambayo inaweza kutekeleza uchunguzi mwafaka.

Ahadi ambayo waziri alitoa ni kwamba kituo hicho kitaimarishwa siku za usoni na kuwa maabara ya kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Kando na hayo, kituo hicho kitatumiwa pia kutekeleza utafiti wa kimatibabu katika michezo, usalama wa kiafya wa wanamichezo, majeraha wanayopata, afya yao ya akili, lishe bora na changamoto zinazotokana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Ustadi wa Kenya ughaibuni katika riadha umeathirika na migogoro ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Sheria za kukabiliana na tatizo hilo zinahitaji kwamba wanariadha wa Kenya wawe wakifanyiwa vipimo kila mara.

Kulingana na ripoti ya mwaka 2022 ya kitengo cha uadilifu katika riadha, wanariadha wapatao 55 wa Kenya wamepigwa marufuku huku wengine 8 wakiwa wamesimamishwa kwa muda.

Website |  + posts
Share This Article