Kituo cha utafiti wa ugonjwa wa Malaria kimezinduliwa katika eneo la Thika, Kaunti ya Kiambu kwa lengo ya kufanikisha mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Mradi huo wa shilingi milioni 380 unaofadhiliwa na serikali ya Ujapani, utatekelezwa na chuo kikuu cha Mount Kenya kwa ushirikiano na chuo kikuu cha Osaka City na Serikali ya Kaunti ya Homa Bay.
Mradi huo unahusisha kuanzishwa kwa maabara maalum ya maswala ya molekuli na maswala ya kinga katika bewa la Thika la chuo kikuu cha Mount Kenya katika Kaunti ya Kiambu na kituo cha utafiti katika Kaunti ya Homa Bay.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika bewa kuu la chuo kikuu cha Mount Kenya huko Thika, balozi wa Ujapani humu nchini Ken Okaniwa amesema inasikitisha kuwa ugonjwa wa malaria bado unawaua watu wengi Barani Afrika licha ya pesa nyingi kutumika kukabiliana nao.
Chansela wa chuo hicho kikuu Dakta Vincent Gaitho alisema kituo hicho cha kukabiliana na ugonjwa wa Malaria kinatoa nafasi kwa wawekezaji kutengeneza dawa na chanjo, kwa kushirikiana na watafiti wengine wa maswala ya Kisayansi.
Mradi huo pia unafadhiliwa na wizara ya afya, wizara ya elimu na shirika la kimataifa la maendeleo la Ujapani,-JICA.